CCM Kilombero yaipongeza REA usambazaji umeme vijijini, vitongojini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:27 PM Jun 26 2025
CCM Kilombero yaipongeza REA usambazaji umeme vijijini, vitongojini

Halmashauri Kuu ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro imeipongeza Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kufikisha umeme katika Vijijini vyote 110 vya Wilaya hiyo pamoja na Vitongoji 283 kati ya 458.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 huku akiwapongeza Madiwani, Wabunge na Watendaji wa Serikali.

“Tuwapongeze sana Waheshimiwa Madiwani, Wabunge kwa kusimamia Ilani ya CCM katika Wilaya yetu kufanikiwa. Lakini pia tuwapongeze sana Watendaji wa Serikali kwa kusimamia maelekezo ya ilani,” alipongeza Mwenyekiti huyo.


Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Wajumbe wa Mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya alimpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kutekelezwa kwa miradi iliyoahidiwa katika Ilani ya CCM katika Wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena aliahidi kuwa Wakala utaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme vinapata umeme ili lengo la Serikali la kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania linatimia.