Jengo jipya Ofisi ya TAKUKURU Kishapu lazinduliwa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 08:18 PM Jun 26 2025
Jengo jipya Ofisi ya TAKUKURU Kishapu lazinduliwa
Picha: Marco Maduhu
Jengo jipya Ofisi ya TAKUKURU Kishapu lazinduliwa

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, amezindua rasmi jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU wilayani Kishapu, katika hafla iliyofanyika, Juni 25, 2025.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Boniphace Butondo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Chalamila alisema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo mpya utachochea ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa TAKUKURU na kuongeza mwitikio wa wananchi kufika kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya rushwa.

“Shukrani kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na ujenzi wa ofisi ili kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Chalamila.

Alisisitiza umuhimu wa kutunza jengo hilo la serikali, huku akitoa rai kwa watumishi wa TAKUKURU kufanya kazi kwa weledi na uadilifu, ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa kabisa nchini.

Aidha, Chalamila alitoa wito kwa shule zote za msingi na sekondari kuanzisha Klabu za Wapinga Rushwa, akisisitiza kuwa ni muhimu kuandaa kizazi cha watu wazalendo na waadilifu kuanzia ngazi ya chini.

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, Chalamila aliwasihi wananchi kutowachagua wagombea wanaotoa rushwa na pia kuacha kuwaomba rushwa wagombea, ili kupata viongozi bora watakaowaletea maendeleo ya kweli.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, alisema kuwa jengo hilo jipya limeweka mazingira rafiki kwa wananchi kufika na kutoa taarifa kwa uhuru, tofauti na awali ambapo ofisi ilikuwa ya kupanga na iliyowafanya baadhi ya wananchi kuhisi woga au kutojisikia huru.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Boniphace Butondo, alisema kuwa TAKUKURU ni chombo muhimu kwa maendeleo ya taifa, na akampongeza Rais Samia kwa kuwezesha ujenzi wa ofisi za taasisi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, alisema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wanajivunia kupatiwa jengo hilo jipya la TAKUKURU na akawataka kulitumia ipasavyo kwa kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyozuia maendeleo ya wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi, Mkurugenzi wa Miliki wa TAKUKURU, Mhandisi Dkt. Emmanuel Kiyabo, alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo ulianza Januari 27, 2024, na hadi kukamilika kwake umetumia jumla ya shilingi milioni 438.3.