Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu yanaendelea kama yalivyopangwa, huku akiwataka wananchi na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika mchakato huo muhimu wa kidemokrasia.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu yanaendelea kama yalivyopangwa, huku akiwataka wananchi na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika mchakato huo muhimu wa kidemokrasia.
Akizungumza leo Alhamisi Juni 26, 2025 wakati akitoa hotuba ya kuhitimisha mkutano wa 19 wa bunge Majaliwa amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi, na serikali itahakikisha kila raia mwenye sifa anapata haki ya kupiga kura au kugombea bila vikwazo.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha wadau mbalimbali kila mmoja kwa nafasi yake, ikiwemo wananchi ambao ni wapiga kura, kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo,” amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa amani na utulivu wa nchi ni tunu ya kipekee ambayo kila Mtanzania anapaswa kuilinda kwa nguvu zote kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha analinda na kuitunza tunu ya amani na utulivu wa nchi yetu. Kwa upande mwingine, serikali itatekeleza wajibu wake wa kusimamia katiba, sheria.
"Pia serikali itasimamia taratibu zote zilizowekwa ili kila mwananchi mwenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa aweze kutimiza haki yake ya kikatiba bila vikwazo vya aina yoyote,” amesisitiza Majaliwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED