NGOs zatakiwa kuzingatia sheria kuepuka taharuki kuelekea uchaguzi 2025

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:33 PM Jun 26 2025
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu, uwazi na uwajibikaji ili kuongeza tija kwa jamii na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Nsajigwa ametoa wito huo leo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Pwani, uliofanyika katika ukumbi wa Resosi uliopo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha.

Katika hotuba yake, Nsajigwa amesisitiza kuwa mashirika hayo ni washirika muhimu wa serikali katika juhudi za kuleta maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo yanapaswa kuwa kielelezo cha amani, mshikamano na maendeleo endelevu.

"Mashirika haya ni nguzo ya maendeleo. Tunayategemea kusaidia wananchi wetu, lakini pia yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhimiza amani, mshikamano na utulivu,” amesema.

Aidha, ameyakumbusha kuhakikisha kuwa yanafuata taratibu na miongozo ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesisitiza kuwa katika kipindi hiki kinachoelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, mashirika hayo yanapaswa kuepuka kufanya shughuli au kutoa taarifa zinazoweza kuleta taharuki.

"Mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi. Naomba niagize kuwa mashirika yote yafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni. Msibadilike na kuwa sehemu ya migawanyiko ya kisiasa au kuchochea taharuki. Tunawategemea katika kulinda amani na utulivu, ambayo ni tunu ya taifa. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuilinda,” amesisitiza Nsajigwa.

Katika kufunga hotuba yake, Nsajigwa ametoa rai kwa mashirika hayo kuendelea kushirikiana na serikali kwa ukaribu, kufuata miongozo yote ya usajili, kuripoti shughuli zao kwa uwazi na kuhakikisha matokeo ya kazi zao yanawanufaisha wananchi moja kwa moja.