Mradi wa maji wakabidhiwa kwa wakazi 14,000 wa Kwadelo, Kondoa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:18 PM Jun 26 2025
Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Kondoa Dk.Ashantu Kijaji akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi wa maji wa Kwadelo, uliofadhiliwa na Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ikiwa ni kusaidia serikali kupunguza changamoto ya maji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Kondoa Dk.Ashantu Kijaji akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi wa maji wa Kwadelo, uliofadhiliwa na Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ikiwa ni kusaidia serikali kupunguza changamoto ya maji.

Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), kwa kushirikiana na shirika la Africa Community Advancement Initiative (Africai), imekamilisha na kuzindua rasmi Mradi wa Maji wa Kwadelo katika Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya SBL katika kuendeleza maendeleo endelevu na ustawi wa jamii kupitia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Sherehe ya uzinduzi imehudhuriwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dk. Ashatu Kijaji, ambaye alikuwa mgeni rasmi. Mradi huu mkubwa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 292 na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 14,750 wa Kata ya Kwadelo.

Mradi huu umehusisha uwekaji wa pampu ya kisasa ya kuvuta maji (submersible pump), ujenzi wa nyumba ya mashine na tanki la kuhifadhi maji la saruji, mtandao mpana wa mabomba ya kusambaza maji, pamoja na vituo 11 vya kuchotea maji vinavyozalisha zaidi ya lita 107,000 za maji kwa siku.

Maji ni uhai. Mradi huu unaakisi imani yetu ya dhati kuwa upatikanaji endelevu wa maji ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. SBL tunajivunia kusaidia juhudi za serikali katika kuziba pengo la huduma ya maji katika jamii zenye uhitaji mkubwa,” amesema Obinna Anyalebechi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL.

Tangu mwaka 2010, SBL imetekeleza jumla ya miradi 28 ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, ikitoa huduma ya maji safi na salama bure kwa zaidi ya Watanzania milioni 2. Mradi wa Kwadelo ni sehemu ya programu ya muda mrefu ya SBL iitwayo "Water of Life", na unalingana na malengo ya kampuni katika nyanja za Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Katika hotuba yake ya uzinduzi,Dk. Ashatu Kijaji aliipongeza SBL kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto ya maji vijijini.

“Ushirikiano wa aina hii ndio tunaouhitaji, ambapo sekta binafsi inakuwa sehemu ya kuleta mabadiliko ya kijamii. Maji siyo tu hitaji, bali ni heshima, afya, na fursa kwa jamii,” alisema Kijaji.

Uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Kwadelo si mwisho, bali ni mwanzo wa maisha bora na yenye afya kwa wakazi wa Kwadelo na maeneo ya jirani. SBL inasisitiza tena dhamira yake ya kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya maji inayobadilisha maisha ya watu kote nchini Tanzania – ikisimamia upatikanaji wa maji, heshima ya binadamu, na maendeleo kwa wote.

SBL pia inatoa wito kwa washirika wa maendeleo, taasisi za serikali na sekta binafsi kushirikiana kwa pamoja katika kusaidia suluhisho za jamii zinazochochea ujenzi wa Tanzania bora zaidi.