Miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mkoa wa Mwanza inaendelea kuimarika, huku walengwa wa mpango huo wakihimizwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ili kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa TASAF pamoja na wenza wa viongozi wa kitaifa walipomtembelea ofisini kwake jana.
"Tunaendelea vizuri na utekelezaji wa miradi ya TASAF, na imekuwa na mafanikio makubwa sana katika mkoa wetu wa Mwanza, ambapo kaya zilizotambuliwa zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka," alisema Elikana.
Aliongeza kuwa yapo makundi mbalimbali yaliyoanzishwa na wanufaika wa mpango huo yanayojihusisha na masuala ya ushirika wa kuweka na kukopa, hatua inayowawezesha kujikomboa kiuchumi, kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni, na kutimiza azma ya Serikali ya kumtoa mwananchi kutoka hali ya umasikini.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango wa TASAF kwa Mkoa wa Mwanza, Mratibu wa mpango huo, Monica Mahundi, alisema kuwa mpango huo unatekelezwa katika wilaya zote saba za mkoa huo, na una jumla ya wanufaika 51,045. Aidha, jumla ya miradi 412 yenye thamani ya Shilingi bilioni 20.2 imetekelezwa.
Mahundi alibainisha kuwa vikundi vya kuweka akiba 3,857 vimeundwa, huku wanufaika walioungana kwenye vikundi hivyo wakiwa 43,224. Kiasi cha fedha kilichowekwa hadi sasa ni Shilingi milioni 840.
Aliongeza kuwa vikundi 16 kati ya hivyo tayari vimepokea mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani, ambapo jumla ya Shilingi milioni 47 zimepokelewa. Halmashauri bado zinaendelea na zoezi la uhakiki ili kuhakikisha vikundi vingine vinapata fursa ya kunufaika na mkopo huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano kutoka TASAF Makao Makuu, Japheth Boaz, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mzirai, alisema wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha azma ya kuikomboa jamii inatekelezwa kikamilifu.
Naye Mwenyekiti wa Wenza wa Viongozi wa Kitaifa (Ladies of New Millennium Women Group), Tunu Pinda, alisema kuwa unapomsaidia mtu mwenye uhitaji kwa kumgusa katika nyanja mbalimbali kama elimu na uchumi, tayari unakuwa umemgusa Mungu.
"Tunafanya kazi ya serikali lakini pia tunafanya kazi ya Mungu, ambayo malipo yake mengine hamuwezi kuyaona hapa. Hapa mtaona mishahara na posho, lakini yale mengine tutayakuta huko mbele ya safari, na mengine tutaona kupitia vizazi vyetu," alisema Pinda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED