Ali Nurdin ‘Six’ ajitosa Ubunge Kondoa Mjini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:10 PM Jun 29 2025
Nurdin Six na familia yake wakati akichukua fomu
Photo: File
Nurdin Six na familia yake wakati akichukua fomu

Makada watano wa Chama cha Mapinduzi (CCM),wamejitokeza na kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania Ubunge wa jimbo la Kondoa mjini, akiwamo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Umma wa taasisi ya mabalozi wa usalama barabarani (RSA)Ali Nurdin maarufu ‘Six’.

Nipashe  iliyoweka kambi katika ofisi za CCM za wilaya ya Kondoa,kuanzia siku ya kwanza ya Uchukuaji fomu imewashuhudia wagombea hao wakiingia na kutoka katika ofisi hizo huku wengi wao wakisindikizwa na mtu mmoja mmoja na wengine wakisindikizwa na familia zao.Hata hivyo Mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo la Kondoa mjini Ali Makoa,hadi leo  saa 10 jioni ikiwa ni siku ya pili ya Uchukuaji fomu,alikuwa hajajitokeza kuchukua fomu.

Akizungumzia mwitikio wa Uchukuaji fomu katika majimbo ya Kondoa Mjinin a Kondoa Vijijini,Katibu wa wazazi wilaya ya Kondoa Juma Koja,alisema hadi kufikia saa kumi jioni leo katika jimbo la Kondoa mjini mbali na Ali Nurdini wagombea wengine waliojitokeza ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Dodoma,Mariam Ditopile,Ismail Said,Mariama Bura na Mhandisi Yusuph Musa

Koja alisema katika jimbo la Kondoa vijijini mpaka muda wa saa kumi jioni walikuwa wamejitokeza watu sita wakiongozwa na  Mbunge aliyemaliza muda wake,Dk Ashatu Kijaji,wengine ni Juma Twaha,Idrisa Isaya,Hamza Mnyau,Said Mnyeke na Suphiani Abdallah.

Akizungumza mara baada ya  kuchukua fomu, ‘Six’ ambaye pia ni mjumbe wa baraza la Taifa usalama barabarani,  alisema chama chao kimeweka mazingira mazuri ya vijana kushiriki katika siasa na kushika nafasi ya uongozi kupitia  uchaguzi na kuwaomba vijana watumie nafasi hiyo kwa ajili ya mustakabali mwema wa nchi.

“Vijana tunapaswa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huu kuanzia kuwania nafasi mbali mbali na mwisho Kwenda kupiga kura na kucahgua viongozi watakaowahudumia kwa maeneleo ya maeneo yetu”alisema Six

Alisema kwa kuwa muda wa kampeni ndani ya chama hazijaanza na wakati ukifika atawaeleza wajumbe,kwanini amedhamiria kuwa mbunge wa Kilombero na kwanini ni muhimu kwao kumuunga mkono katika hatua hiyo kwa ajili ya maslahi mapana ya jimbo la Kondoa.