Wakili Kidyalla ajitosa Ubunge Dodoma Mjini

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 11:15 AM Jun 29 2025
Wakili Eric Kidyalla akichukua fomu
PICHA: RENATHA MSUNGU
Wakili Eric Kidyalla akichukua fomu

Wakili Eric Kidyalla amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania kugombea Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Jimbo la Dodoma Mjini.

Kidyalla ameungana na wajumbe wengine mbalimbali  mkoani hapa  waliojitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania ubunge katika jimbo hilo la Dodoma mjini ambalo limegawanywa.

Akizungunza mara baada ya kuchukua fomu hiyo,Kidyalla amesema sababu iliyomsukuma kuchukua fomu hiyo ni pamoja na kuwa yeye ni kada wa Chama hicho hivyo ameona ni vyema kutumia haki yake ya kikatiba kugombea nafasi hiyo.

"Nimechukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hii,lengo ni kutaka kuendeleza mambo mazuri ya maendeleo yaliyoachwa na mbunge aliyepita katika jimbo hili kabla ya serikali kuamua kuligawanya jimbo hilo na kutoa fursa ya wagombea wengi kujitokeza kuchukua fomu,"amesema Kidyalla.


Amesema anaamini atafanya vizuri katika kinyang'anyiro hiko na kuongeza kuwa endapo atafanikiwa atashirikiana na viongozi wengine kwa ajili ya kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi pamoja na wanadodoma wote.


Mbali na hayo mgombea huyo pia ameishkuru serikali kwa kuridhia Jimbo la Dodoma mjini kuweza kugawanywa jambo ambalo limetoa fulsa kubwa kwa makada wa CCM wengi kujitokeza kugombea nafasi ya Ubunge.

"Jimbo la Dodoma mjini kijiografia lilikuwa kubwa hivyo kuridhiwa ligawanywe,  Rais, Samia Suluhu amefanya jambo jema na litatoa fursa kubwa kwa wananchi,"amesema Kidyalla.