Mwanasheria Zanzibar ang'aka kuhusu matangazo wagombea

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:49 AM Jun 29 2025
MWANASHERIA mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Omar Said Shabani.
PICHA: RAHMA SULEIMAN
MWANASHERIA mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Omar Said Shabani.

MWANASHERIA mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Omar Said Shabani,amesema tamko la Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja Idrisa Kitwama Mustafa ya kuwataka wagombea wote wa vyama vya siasa kutobandika matangazo ya makaratasi katika mkoa huo na badala yake kuweka matangazo ya kidigitali tammko hilo ni batili na ni kinyume na sheria namba nne ya uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 29 katika Ofisi za chama hicho Vuga Mjini Zanzibar Mwanasheria huyo alisema chama kinashtushwa na ukimya wa Tume za uchaguzi na kufumbia macho matamshi ambayo yanapotosha sheria za uchaguzi ambapo wameapa kusimamia sheria na katiba ya nchi.

Alisema kauli hiyo wanaiweka katika muktaza wa kupotosha mamlaka ya tume ya uchaguzi chini ya kifungu cha tisa cha sheria ya uchaguzi.  Alisema kwa mujibu wa sheria mambo yanayohusu vifaa vya kampeni yanafanywa kwa muungozo unaotolewa na tume ya uchaguzi. 

"Kifungu cha 64 cha sheria ya uchaguzi tume itatayarisha muungozo wa ubandikaji na uchapishaji wa vifaa vya kampeni na sheria inatambua matangazo ya kampeni yatakua ni yamakaratasi"alisema.

Mwanasheria huyo alisema hakuna muungoozo wa tume wa kukataa matangazo ya karatasi na kama utakuwepo watapinga Mahakamani kwa sababu ni kinyume na sheria au wabadilishe sheria ya uchaguzi. 

Omar ambae pia ni waziri wa biashara na maendeleo ya viwanda aliwatoa hofu wagombea wote wa vyama vya siasa kuhusu tamko hilo ambalo alisema ni batili. Alisema hawapingi matumizi ya kidigitali lakini isiwe kikwazo ya kuwanyima fursa wengine ambao hawana nyenzo na uwezo wa kutangaza matangazo yao kwa njia za kidigitali.

Mkuu wa Mkoa Kitwana hivi karibuni alitoa tamko la kukataa katika mkoa huo kubandikwa kwa matangazo ya makaratasi ya wagombea na badala yake kuweka matangazo ya kidigitali ili kulinda mazingira na mji kuwa na haiba nzuri.