TAASISI ya Elea Foundation na ile ya Nordic Impact Funds, imetoa uwekezaji mpya kwa kampuni inayojihusisha na masuala ya teknolojia ya kilimo ili kusaidia kuimarisha huduma za ugani kidijitali katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Uwekezaji huo pia utasaidia kutengeneza mtandao wa maafisa ugani yaani Uber ya maafisa ugani, ikiwa ni pamoja na kuzindua jukwaa la masoko ya wakulima kidijitali liitwalo Cropsupply.com
Akizungumzia kuhusiana na uwekezaji huo Afisa Mtendaji Mkuu wa MazaoHub, Geophrey Tenganamba amesema kuwa uwezeshaji huo,utawawezesha wakulima kupata huduma kidijitali kwa usaidizi wa karibu na maafisa ugani ikiwa ni Pamoja na kuwezesha wakulima kuuza Mazao kwa uwazi, kwa faida na kwa uhakika ndani na nje ya Tanzania.
Amefafanua zaidi ya kuwa kuhusiana na namna uwekezaji huo umeisaidia kampuni yake ya Mazao Hub kutekeleza majukumu yake, Tenganamba alisema kuwa kampuni hiyo imeanzisha Jukwaa linalowaunganisha wakulima na masoko lijulikanalo kama CropSupply.com,ambalo wakulima, wanunuzi, wasafirishaji na wafanyabiashara wa mazao wanapata taarifa sahihi kuhusiana na upatikanaji wa Mazao kila nchi, kila mkoa na kila Kijiji.
Mbali na hilo amesema kuwa Pamoja na kuzalisha ripoti ya uzalishaji yaani traceability reports zinazohitajika zaidi na wanunuzi kutoka nje.
“Hakika chini ya uwezeshwaji wa Wizara ya Kilimo kampuni yetu ya Mazao Hub ambayo ni kati ya matokeo ya mradi wa BBT imekuwa ikipata uwekezaji kutoka kwa wadau tofauti ambapo kwa sasa uwekezaji huu unaiwezesha kampuni kuyafungua masoko ya wakulima kwa njia ya kidigitali hususani katika kuagiza na kufanya biashara ya mazao kwa chini ya mfumo wa cropsupply.com," amesemaTenganamba.
Pia anabainisha zaidi kuwa mfumo huo utawezesha wakulima wa hapa nchini kuuza bidhaa zao nje ya nchi, ambapo kwa sasa mfumo unafanya kazi katika nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya na Zambia kwa kuwa nchi hizi zinafanya kazi kwa ukaribu zaidi na Tanzania katika sekta ya kilimo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED