TRA yapata mwarobaini pombe feki sokoni

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:21 AM Dec 04 2024
Kamishna Mkuu wa TRA, Yussuf Mwenda.
Picha:Mtandao
Kamishna Mkuu wa TRA, Yussuf Mwenda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetengeneza stempu maalumu za kielektroniki (ETS) kwa ajili ya vinywaji vikali kudhibiti pombe feki sokoni.

Aidha, imekusanya Sh. trilioni 12.33 kuanzia Julai hadi Novemba, mwaka huu, ikiwa ni zaidi ya lengo lililowekwa kwa asilimia 105. Katika kipindi hicho, TRA ililenga kukusanya Sh. trilioni 12.30.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yussuf Mwenda, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, kwenye mafunzo namna mamlaka inavyofanya kazi zake.

Alisema mamlaka imetengeneza stempu zenye alama nyingi za ulinzi ili kukabiliana na bidhaa bandia hasa vinywaji.

“Tumetengeneza stempu mpya zenye alama za ulinzi ambazo si rahisi kuzinakili. Hii tunaamini itatuongezea mapato na itapunguza tatizo la bidhaa feki hasa pombe sokoni,” alisema. 

Alisema TRA inaendelea kutoa elimu na kufuatilia kwa wafanyabiashara wasiotumia stempu sahihi, ili kudhibiti pombe feki.

Kuhusu makusanyo, alisema ni ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Katika kipindi hicho, TRA ilikusanya Sh. trilioni 10.80.

Alisema makusanyo hayo yamechangiwa na mamlaka kuongeza ufanisi na kuboresha uhusiano kati yake na walipakodi, yakiwamo mawasiliano na majadiliano na wafanyabiashara na ongezeko la walipakodi wapya.

“Tumeongeza Sh. trilioni mbili ndani ya miezi mitano, hii ni kazi kubwa. Tumejenga mazingira ya kuhakikisha walipakodi wanalipa bila kushurutushwa. Kipekee niwashukuru walipakodi wote,” alisema Mwenda.

Alisema mapato ya forodha yameongezeka kutoka wastani wa Sh. bilioni 850 kwa mwezi, hadi Sh. trilioni 1.2 na Sh. trilioni 1.15 Oktoba na Novemba mwaka huu, mtawalia.

Mwenda alisema ongezeko la mapato ya forodha limechangiwa na ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam, baada ya kampuni ya DP World kuanza kazi, hasa suala la uondoshaji wa mizigo bandarini na kupungua kwa muda wa kuhudumia meli.

Mwenda alisema mamlaka hiyo inakusudia kuajiri watumishi 1,000 mwakani, ili kuongeza ufanisi hasa usajili wa walipakodi wapya.

Alisema kuanzia Januari mwakani, TRA itaanza kufanya makadirio ya tozo za forodha kwa mfumo mpya ambao utakuwa bora kuliko uliopo.

Alisema TRA inakusudia kuimarisha mifumo yake ili kuwezesha wafanyabiashara na walipakodi wengine, kupata huduma mtandao kwa uhakika na ndani ya muda mfupi.

Lengo, kwa mujibu wa Mwenda, ni kuongeza pato la taifa (GDP) kupitia kodi kutoka asilimia 13 ya sasa hadi asilimia 15.

Kuhusu matumizi ya risiti za kielektroniki, Mwenda alisema TRA imeimarisha mfumo wa ukaguzi wa mashine hizo kupitia mfumo wa EFDMS, ambayo inampa uwezo mtumishi wa mamlaka hiyo, kuona mfanyabiashara ambaye hajatoa risiti kwa muda mrefu na kuwasiliana naye ndani ya mfumo.

“Kwa hiyo kutosikia malalamiko sio kwamba hatukagui. Tumebadilisha staili, tunakwenda moja kwa moja kwa mhusika wanaangalia ni kina nani ambao hawatoi kabisa anafuatwa yule ndani ya mfumo kuulizwa kwa nini hatoi risiti na hii inatusaidia kuondoa malalamiko,” alisema.

Hata hivyo, alisema TRA inakabiliwa na changamoto za baadhi ya wafanyabaishara kukwepa kodi pamoja na ukosefu wa mashine za ukaguzi katika mipaka ya Tunduma upande wa Zambia, Kasumulo na Namanga, inayochangia msururu mrefu wa malori yanayovuka kwenda nchi jirani.

“Mfano, kuna watu wanaanzisha biashara ili auze risiti za EFD, tumetengeneza kitengo kizuri cha uchunguzi, tunasaidiwa na vyombo vya ulinzi kuwabaini. Tukiwabaini tutarejesha kodi yetu yote na riba, pia tutawashitaki. Niwakumbushe wafanyabiashara, hakuna biashara ya kuuza risiti. Timu iko mtaani inafanyakazi na hivi karibuni kutakuwa na matokeo makubwa sana,” alisema.

Alisema changamoto nyingine ni magendo kwenye mipaka ya nchi, inayochangiwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya ukaguzi mizigo mipakani.

Alisema katika mpaka wa Tunduma, wamekubaliana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), kusaidia kununua mashine upande wa Nakonde Zambia, ili kuondoa foleni ya malori Tunduma.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, aliielekeza TRA kuanza na mpaka wa Namanga, mkoani Arusha ili kuendana na kasi ya huduma inayotolewa upande wa Kenya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza, aliipongeza TRA kwa kuongeza makusanyo ya mapato na kueleza kuwa Bunge linatamani kuona ongezeko la mapato litakaloiwezesha serikali kupunguza kukopa.

“Ushauri wetu wa muda mrefu ni kwamba TRA iwekeze kwenye mifumo ambayo inasomana ili kuongeza mapato. Tunaamini kwamba mifumo ikiwa mizuri, hiki kinachokusanywa kitaongezeka hata mara mbili.