Waziri Masauni katika wakati mgumu

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:34 AM Sep 10 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni

HAMAD Masauni yuko katika wakati mgumu, akishinikizwa kujiuzulu cheo chake cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na matukio ya mauaji, utesaji na utekaji yanayoendelea nchini.

Kukiwa na shinikizo hilo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya kimahakama kuchunguza matukio ya watu kutekwa, kuteswa na kuuawa yanayoendelea kuripotiwa nchini. 

Shinikizo la Waziri Masauni kuachia ngazi lilikolea zaidi jana wakati wa mazishi ya Ally Kibao, Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa chama hicho yaliyofanyika nyumbani kwake, Sahare, mjini Tanga na maziko yake kufanywa katika Kijiji cha Tarigube, Kata ya Togoni saa tisa alasiri.

 Kibao anadaiwa kuwa jioni ya Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Kibo Complex Tegeta, Dar es Salaam, akiwa safarini kuelekea nyumbani kwake Sahare, Tanga na basi la Tashrif, alishushwa na watu waliokuwa na bunduki.

 Asubuhi ya Jumamosi iliyopita, mwili wake ulikutwa maeneo ya Ununio, Tegeta ukiwa na majeraha makubwa, ikiwamo usoni.

 Akiwa kwenye msiba huo jana, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alimwomba  Rais Samia aunde tume ya kimahakama ili ichunguze matukio ya utekaji, utesaji na mauaji yanayoendelea kwa kuwa yeye pekee ndiye mwenye mamlaka hayo.

 Alisema chama hicho kinaamini kuwa njia hiyo ndiyo pekee inayoweza kusaidia ili hata wale wenye ushahidi ambao hawawezi kuutoa kwa polisi, watautoa kwa tume hiyo.

 Alidai kuwa baadhi ya watu wanaotekeleza vitendo hivyo, serikali inawafahamu kwa kuwa alishawahi kutaja baadhi ya majina katika mkutano na waandishi wa habari, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

 Alisema hakubaliani na kauli ya Rais kuelekeza Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo ilhali lenyewe ndio watuhumiwa namba moja wa chama hicho.

 "Leo mnaweza kuona kuwa amani hii inayumba katika msiba huu, kuna siku amani hii msipoangalia itayumba katika mitaa yote ya nchi hii," alionya.

Mbowe alisema kuna Watanzania wengi wanapotea, wakijumuisha waojihusisha na wasiojihusisha na siasa, hali kadhalika wafanyabiashara.

 "Tume ya kijaji ya kimahakama ndio chombo pekee kinachoweza kuyahoji makundi yote kikamshauri Rais hatua za kuchukua na kuwabaini wahalifu," alisema.

 Alidai kuwa ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama, mna watu wema, lakini miongoni mwao, wamo pia watu ambao ni wahalifu wa kutisha.

 VURUGU MSIBANI

Wakati Waziri Masauni anaanza kuwasilisha salamu za pole kwa dua ya kumwombea marehemu, baadhi ya waombolezaji walisikika wakimzomea na kumtaka asiendelee, huku wengine wakisema, "Masauni jiuzulu... Masauni aondoke..."

 Ni hali iliyomlazimu Mwenyekiti Mbowe kuingilia kati na kuwasisitiza watu hao watulie ili amalizie hotuba yake ili mambo mengine yaendelee.

 "Ninataka kutoa rai kwa wana CHADEMA, tusiwe sababu ya kuvuruga msiba huu, ajenda yetu tunayoidai tutaendelea kuidai, lakini lazima turuhusu msiba huu uendelee kwa utulivu," alisema.

 Akiendelea na hotuba hiyo, Masauni alisema  serikali na Rais Samia wamesikitishwa na tukio  hilo na kuagiza uchunguzi ufanyike haraka ili wote waliohusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

 Aliwahakikishia waombolezaji kuwa serikali haitoliacha suala hilo "liende hivi hivi" na maelekezo ya Rais yameshaanza kufuatwa na hatua zitachukuliwa kwa watakaobainika.

 "Tumesikitishwa sana na kuhuzunishwa na kusononeshwa, ni jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi yetu ambayo miaka yote tumekuwa tukijivunia usalama na amani kulinganisha na nchi nyingine zinazotuzunguka," alisema.

Mwenyekiti CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alisema alitegemea waziri huyo pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Camilus Wambura kujiuzulu kufuatia kuendelea kuwapo kwa matukio hayo ya kinyama.

 "Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, usiende tena kwenye msiba wa mtu aliyetekwa, nenda kwenye msiba wa mtu aliyeuawa bila kutekwa, mnatuumiza, Nilitegemea baada ya kauli ya Rais jana (juzi), wewe leo (jana) uwe umejiuzulu, IGP awe amejiuzulu na viongozi wengine wakae kando," alisema.

 Lema alisema kuwa aliposikia taarifa za kukamatwa kwa kada huyo, alihisi kuwa ni jambo la kawaida na angeachiwa baada ya muda mfupi, lakini taarifa za kifo ziliumiza moyo wake.

 Alimweleza Waziri Masauni kuwa jana alipokea ujumbe katika simu yake, unaompa angalizo kuwa kama mwezi huu utaisha bila yeye na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, kutekwa na kuuawa, basi wamshukuru Mungu.

 Alishauri serikali kutoruhusu mambo hayo kuendelea kufanywa nchini kwa kuwa maisha ya wanasiasa yamekuwa magumu, wakitembea na wasiwasi kuwa muda wowote wanaweza kutekwa na kuuawa na kuziacha familia zao.

 Aliwashauri wananchi kushikamana na kukemea jambo hilo kwa pamoja badala ya kuachia CHADEMA pekee yake kwa kuwa yakiachiwa, hata wahuni wanaweza kuendeleza vitendo hivyo wakijua kuwa hayajaliwi na serikali.

 Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alimweleza Waziri Masauni kuwa anaunga mkono kauli za viongozi waliojitokeza kuhoji uwajibikaji wake kwa sababu matendo hayo yanatokea katika wizara ambayo anaongoza na hakuna kinachofanyika kuyakomesha.

 Alisema kuwa Kibao hakuwa maarufu, lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kitaalamu katika kazi, akisisitiza "ndio sababu ya kutekwa na kuuawa", akivinyooshea kidole vyombo vya dola kwa madai kuwa huenda vimehusika.

 Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, alisema matukio kama hayo yanazusha hofu kwa wananchi kuhusu usalama wao na kumshinikiza waziri huyo ajiuzulu kwa kushindwa kuyadhibiti.

 Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Balozi Batilda Burian, alisema amesikitishwa na msiba huo na kuwataka wananchi wa mkoa huo kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Kibao ili ampokee na amsamehe dhambi zake.

 Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Wilson Elias, alitaka serikali kukaa pamoja na vyama vya siasa nchini ili kutafuta suluhisho la kukomesha vitendo hivyo kabla havijaamua kuomba msaada kimataifa.

 Alisema matukio hayo ya kutisha yanayolenga zaidi wanasiasa kutoka vyama vya upinzani, hayawakatishi tamaa wala kuwarudisha nyuma katika harakati zao za kutetea maslahi ya Watanzania.

 CCT YAKEMEA

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) pia imelaani vikali tukio la kuuawa kwa kada huyo wa CHADEMA na kusisitiza kuwa matukio ya utekaji na mauaji yafike mwisho kwa kuwa yanaumiza jamii ya Watanzania.

 Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani (KKKT) na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk. Fredrick Shoo alisema wamesikitishwa na mauaji na ukatili wanaofanyiwa Watanzania wasio na hatia.

 "Mnaofanya hayo, iwe kwa sababu yoyote ile, mjue yupo Mungu, nasi tunamwomba adhihirishe wazi uwezo na mamlaka yake, Mungu hadhihakiwi," alisema.

 Askofu Dk. Shoo alitoa wito kwa Watanzania waombe kwa dhati na kukemea vitendo hivyo vinavyotaka kutishia usalama, haki na amani ya nchi.

 Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeunga mkono hoja ya CHADEMA kumwomba Rais kuunda tume ya majaji kuchunguza wimbi la utekaji na mauaji, ambalo lilianza kwa mtu mmoja mmoja sehemu mbalimbali nchini.

 Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile ilieleza kuwa matukio hayo yalianza kwa watoto na sasa watu wazima wanashushwa katika magari ya abiria na kuuawa.

 TEF pia imeutaka uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika ngazi zote, ujitafakari iwapo unastahili kuendelea kuwapo wakati tuhuma hizi nzito za watu kutekwa zikiendelea kusikika sehemu mbalimbali nchini pamoja na kuwekwa wazi majina ya wanaofanya uchunguzi huo.

 Ubalozi wa Marekani nchini pia umetoa wito kufanyika uchunguzi huru na uwazi na haraka kuhusu utekaji unaoendelea na mauaji ya Kibao kwa kuwa matukio hayo hayapaswi kupewa nafasi katika demokrasia ya Tanzania.

 "Mauaji na kupotea kwa watu pamoja na kukamatwa, kupigwa na juhudi nyingine za kuwaengua raia katika uchaguzi zilizotokea mwezi uliopita, havipaswi kuwa na nafasi katika demokrasia," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani nchini.

 Vilevile, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelaani tukio la mauaji ya kada huyo CHADEMA, ikisisitiza inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

 Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu alisema wanatambua tamko la Rais Samia, lakini wao kama tume, wanaendelea na uchunguzi na baadaye watatoa tamko lao.

 Alisema tume hiyo pia inaendelea na uchunguzi wa matukio mengine ya kikatili yanayofanywa na watu wasiojulikana nchini na kukatisha uhai wa watu, akisisitiza vitendo hivyo havikubaliki mbele ya jamii.