WIZARA ya Afya inasubiri mapendekezo kutoka Kamati ya Kitaifa ya Masuala ya Chanjo (NITAG), ambayo itapitia na kutoa maoni kuhusu gharama, ubora na upatikanaji wa chanjo za kudhibiti malaria nchini.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya, Dk. Samwel Lazaro, alisema kuwa chanjo mbili za malaria – RTS, S na R21 – zinaoendelea kupitia mchakato wa mapitio, zinasubiri kupitishwa na Timu ya Wataalam ili kuanza kutumika rasmi nchini.
Dk. Lazaro alifafanua kuwa Wizara ya Afya inategemea maoni ya kitaalam kutoka Kamati ya Kitaifa ya Masuala ya chanjo ili kufanikisha utoaji wa chanjo hizo, hasa kwa watoto chini ya miaka mitano, ambao ni waathirika wa ugonjwa wa malaria.
Alisema chanjo ya RTS, S, inayotengenezwa na kampuni ya GSK kutoka Ubelgiji, bado haijakidhi vigezo vya usajili vinavyotakiwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na kwamba serikali inasubiri mtengenezaji kumaliza mchakato wa usajili.
Chanjo ya R21, ambayo ilipata usajili rasmi Julai 2024, pia inahitaji kupitia mchakato wa tathmini ya kitaalam kutoka kwa Kamati ya Kitaifa ya Masuala ya Chanjo kabla ya kuanza kutumika.
"Tunazingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu utolewaji wa chanjo na tunasubiri ripoti ya Kamati ya Masuala ya Chanjo ili kupata ushauri wa kitaalam kuhusu ubora, gharama, upatikanaji na usalama wa chanjo hizi," alisema Dk. Lazaro.
Akizungumzia jitihada za kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria, alisema takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2022, zinaonesha kuwa kati ya watu 100, ni wanane pekee waliobainika kuwa na vimelea vya malaria.
Alisema hiyo ni hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya 1990, kati ya watu 100, watu 50 hadi 60 walikuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Dk. Lazaro alisema kuwa hatua hizo za kupunguza maambukizi ni matokeo ya juhudi za pamoja za serikali, pamoja na mikakati ya kinga na matibabu, alisema bado kuna umuhimu wa kuendelea na juhudi za kudhibiti ugonjwa huo, hasa kupitia utoaji wa chanjo.
Alisema Serikali pia inaendelea kuimarisha juhudi za kinga na matibabu ya malaria, katika mwaka wa fedha 2024/2025, kiasi cha Sh. bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa za viuadudu katika kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya mbu wanaoeneza malaria kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.
Aidha, Shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa pampu za kunyunyizia viuadudu vya kibaiolojia.
Alisema kuwa kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa malaria husababisha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 75 hadi 80.
Kutokana na hali hiyo, serikali inaendelea kutoa vyandarua vya mbu kwa watoto na wajawazito, kuhamasisha usafi wa mazingira, kufukia madimbwi yenye maji yaliyotuama na kutumia viuadudu vya kibaiolojia kudhibiti viluilui vya mbu.
"Serikali pia inaendelea kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wa malaria na inahimiza wananchi kupima afya zao kabla ya kutumia dawa. Si kila homa ni malaria, hivyo tunawasihi wananchi kupima na kuhakikisha wanakamilisha dozi zao ili kuepusha usugu wa dawa," alisisitiza Dk. Lazaro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED