JUMANNE wiki iliyopita katika safu hii ilijadili mada na picha pana ya elimu nchini, pia mustakabali wa kusuasua kwake.
Ilitajwa nguzo tatu kuu ya mfumo wowote wa elimu, ambayo mlengwa wake ni anayesoma. Inajengwa na jozi ya kwanza ambayo ni serikali, pia wote wanaomiliki mfumo wa elimu kama shule.
Pili, kuna jozi ya walimu na wazazi wanaowajibika maudhui ya mtaala wa masomo, uzame katika uelewa wa msomaji; na nguzo ya tatu ndio inamhusu mwanafunzi anayelengwa.
Katika kufanikisha malengo hayo, kila mmoja wao ana wasifu katika wajibu wa msingi na nafasi yake katika kufanikisha azma hiyo mahsusi.
Ilishafafanuliwa katika makala ya Jumanne wiki iliyopita, kwamba tafsiri ya elimu inabaki kwa nafasi ya kujifunza ujuzi, maarifa na uelewa mpana.
Namna ya uwasilishaji wake, inakuwa imeandaliwa mpango mpana unaoitwa mtaala, huku kuna miongozo ya uwasilishaji, inayogusa cha kufanyika kila siku, kwa jina la muhtasari wa masomo (syllabus)
MWANAFUNZI ANAVYOWAJIBIKA
Kwa mujibu wa tafsiri ya kamusi mwanafunzi ni “mtu anayejifunza elimu au kazi fulani...”
Inapokuwa mwanafunzi analitafuta hilo katika mfumo rasmi, kunapaswa aandaliwe katika nafsi yake kabla ya kuanza kupokea elimu husika shuleni.
Kwa maana hiyo, mwanafunzi anajengewa mambo mawili makuu; kuwa na wasifu unaomuunda kwa utayari wa kusoma, pia stadi za kupokea elimu anayoandaliwa, ili lengo litimie.
Ndani yake inatajwa wasifu wa nje wa mwanafunzi kwamba ni kuwa na utii na nidhamu, nadharia inayotumika hata kwa kada za askari.
Utii ni hali ya kuwa na msimamo chanya kwa maelekezo yote yanayomhusu, huku nidhamu inahakikisha unyeyekevu wake katika kushughulikia yote sahihi katika kufanikisha upatikanaji elimu kwa mwanafunzi huyo.
Kwenye utii na nidhamu, kunakuwapo baadhi ya nyenzo zinazotumika kufanikisha, mojawapo ni sare mahsusi katika mfumo huo wa shule
Sare zinaweka baadhi ya sifa kwa mwanafunzi kama vile kumtambulisha kwa umma, kwamba yu mwanafunzi na jamii inatakiwa kumpa haki yake ya uanafunzi,
Hiyo inajumuisha haki zake kama vile kulipa nauli mahsusi kwenye mabasi ya umma iliyopangwa na serikali kwa nafasi yake.
Pia, sare zinabaki kuwa kinga kumuongoza mwanafunzi katika kanuni za usafi anazopaswa kufuata, hali kadhalika inamuengua kutoka makundi yasiyoendana na uanafunzi wake.
Mwanafunzi huwa anafunzwa kutii ratiba na kanuni za muda, ambazo ni muhimu kwake kwa wakati huo na maisha yake baadaye, iwe kazini hadi nyumbani.
Vilevile kinachoendana na hoja ya utii na nidhamu kwa maagizo au kiuzazi, iwe kutoka kwa walimu na walezi wengine, nyenzo tajwa inatumika kwa mtazamo uliokusudiwa.
Mjumuisho wa ngazi hiyo kabla ya kuingia darasani, inakuwa imefanya kazi ya kumuandaa mwanafunzi kupokea ya mwalimu, akili na mawazo akiwekeza kwa utii na nidhamu kunyenyekea mchakato wa darasani.
Hapo kimantiki anakuwa kajiweka vizuri kufunzwa, naye kujifunza kulingana na njia akatazokuwa ameandaliwa.
Maana yake hapo mwalimu mhusika anakuwa katika nafasi bora ya kuwasilisha nadharia na maelekezo yake kwa mpokeaji, mwanafuzi,
Katika nafasi yake mwalimu anabaki na kikwazo kimoja pekee cha pale panatokea sababu zilizo nje ya uwezo wake darasani, ingawa katika sura ya pili, bado ana stadi na mamlaka yake ya kiualimu kutimiza azma tajwa, akishirikiana na wadau wengine kama wazazi na uongozi wa kishule.
Vikwazo vinaweza kuwa kama kiwango cha uwezo binafsi wa mwanafunzi kunasa anayofunzwa, shida ya miundombinu ya kusoma na matatizo ya nyumbani anakotoka na hata nidhamu.
ANAKOSIMAMA MWALIMU
Katika mfumo wa masomo, mwalimu ana jukumu la kufikisha maudhui ya kinachopangwa kwa mwanafuzi kukijua katika taaluma, mahsusi kutoka katika mtaala wake.
Mwalimu huyo katika jukumu lake, pia ana lingine la kubaki mlezi wa mwanafunzi darasani, hata nje ya darasa, akiwa kwenye himaya hiyo.
Hapo mwalimu anachukua wasifu wa mzazi wa pili wa mwanafunzi muda wote awapo masomoni.
Ni moja ya sababu katika shule nyingi kimuundo, kunakuwapo mwalimu wa utawala wa nidhamu, pia mwingine mahsusi kwa utawala wa taaluma.
MAISHA YA DARASANI
Masomo yanapoendelea darasani, daima ni himaya ya wawili, mwalimu mahsusi katika somo lililoko kwenye ratiba na mwanafunzi.
Humo kunatawaliwa na mambo kadhaa, mwalimu akitumia stadi na njia za kupitishia masomo yake kumfikia mwanafunzi.
Mojawapo ni kwamba, muda wote mwalimu anatakiwa kumuelewa kwa kina mwanafunzi wake, kuanzia saikolojia na matendo yake nje na ndani ya darasa, hadi hulka na uwezo wake katika mapokeo ya taaluma.
Mwalimu hutumia maelezo na mtiririko wa lugha unaoambatana na uwezo na saikolojia ya mwanafuzi katika maisha ya kila siku.
Mfano ni kumbaini kama ana huzuni siku hiyo na sababu ya hali hiyo, ili kufanya kazi ya kumrudisha katika mtiririko wa kupokea taaluma.
Ni aina ya mambo yanayofanywa katika taaluma ya ualimu, ndio maana kozi zao hazikosi masomo au maudhui ya: Sosholijia ya wananafuzi, kujua namna wanavyojichanganya katika jamii.
Pia, kozi ualimu hufunza Saikilojia yao, hali kadhalika Falsafa ya mwanafunzi, ambavyo vyote vinazama katika maudhui ya fikra na mantiki ya kufikiri.
Jambo ligine la mwalimu anapowasiliana na wanafunzi darasani kuwafunza, anatakiwa kufanya tathmini wakati wote akitumia vigezo mbalimbali kama; macho yao, mwitiko anapowauliza, uandikaji, hata wanavyokaa vitini
Mjumuisho wake, humpatia mwalimu uelewa wa wanafunnzi walivyo, wakati kipindi kinaendelea au baada ya jumla ya vipindi fulani.
Hilo huendana na kuwapa majaribio mbalimbali wanafunzi baada ya vipindi kadhaa vya masomo, au hata kabla ya kuanza mada mpya.
Pia, kuna maswali na mtindo wa uwasilishaji hutegemea somo, kiwango cha darasa, aina wanafunzi na mazingira.
Mara zote sifa ya mwalimu ni kuwa rafiki darasani kuwafanya wanafunzi wawe tayari kupokea mada tajwa, ikijumuisha mbinu kama vichekesho na mifano ya mambo wanayoyafamu au yaliyoko maisha mwao.
Hata inapofika hatua ya ngazi ya mwisho iwe muhula au ngazi fulani, suala la haki ya kuulizwa maswali lina nafasi yake, ili kutoa uhalisia wa ngazi ya uelewa, ikiwa inaamuundia msaada mwalimu penye ngazi nzuri zaidi ya maboresho.
Ni sura nyingine kama itolewayo darasani, kwamba mwanafunzi hupewa fursa ya kuuliza asikoelewa.
Anayefanya vibaya mtihani, badala ya kushutumiwa kiadui, kisaikolijia ni mhitaji wa ushirikiano kukomboa kasoro zake kwa azma ya kujenga, ili kufikia ufanisi kwa kupewa usaidizi.
Katika uendeshaji wake, nadharia ya kiutawala ambayo inaelimisha kutumika mwongozo rafiki kiutendaji huwa ni kipaumbele wahusika wakijiongoza au kuhamasika kuelewa.
Mtaalamu wa menejimenti aitwaye Mc Gregori, alibuni nadharia hiyo na kuibatiza jina nadharia Y.
Ngazi ya pili ya usimamizi huo inaitwa, Nadharia X, ambayo iko jirani na usimamizi wa karibu, hata amri.
Hiyo inatajwa kuwa muhimu kimenejimenti, pale nadharia ya kwanza ya kuhamasishana inakwama.
Katika menejimenti ya darasani, nayo inatumika hasa mwanafunzi anapoonyesha utukutu na ndio hasa kanuni ya kutumia viboko shuleni kuna wakati inachukua nafasi yake.
Viboko na miongozi yake vinapatikana kupitia Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, ikilenga kumrekebisha mwanafunzi kinidhamu.
WANAKWAMA WAPI?
Mwalimu katika utendaji ni kisiwa, ila anakabiliwa na wimbi la tabia hasi nje ya shule na ikipenya ndani yake, iwe shule ya bweni au kutwa.
Mmojawapo wa wakala mkuu wa kuvusha hayo mabaya ni nyenzo za mitandao jamii na udhibiti duni wa wazazi na walezi, pia wanafunzi hao huzama katika matendo hasi kama utoro darasani, matumizi ya dawa za kulevya kama bangi.
Vilevile, hali halisi ya maisha, mfano kwa wazazi ambao wametingwa na ratiba ngumu kimaisha, ikiwamo katika miji mikubwa, wanakosa hata muda wa malezi kwa watoto.
Kuna wazazi wajasiriamali wanaokuwa katika kazi zao tangu kukucha asubuhi, hadi kiza kinene, wanatumia muda wa kulala, kitaaluma wanabakiwa na jukumu la kufadhili mahitaji pekee, yote yanambakia mwalimu.
Hiyo inaenda hata kwa wazazi wakulima wanaohamia mashambani katika baadhi ya msimu, huku walezi mitaani kama madereva wa bodaboda wenye tabia ya kuhadaa mabinti kuingia katika wimbi la mapenzi, wakitumia pengo la umasikini wao.
Pia, wako baadhi ya walimu wenye kasoro zao, kukiwapo jukumu la kundi lililoweka kando malezi ya utii na nidhamu kwa mwanafunzi, wakibakiwa na jukumu la ufundishaji darasani, tena wakilipua, baadhi yao wanajenga fursa ya kupata wateja wa tuisheni.
Ni wiki iliyopita tu kukawapo taarifa ya kipolisi, mkasa wa binti kubakwa na mkuu wake wa shule, tendo likifanyika katika ofisi ya makamu wake.
Inabaki kuwa majibu, kwa kurejea miaka ya nyuma, ofisi za wakuu hao, ikiongezewa na ile ya mkuu wa nidhamu, kama ilivyo ofisi ya walimu, ilitawala kihisia ina ‘harufu’ ya nidhamu na utii kwa mwanafunzi.
Sifa yake ilikuwa “penye usalama kumsaidia kila mwanafunzi mhitaji,” lakini sasa inageuka ulingo wa kashfa ya kitaifa na sio tukio la kwanza kusika kutoka shule tofauti.
Sasa inawaacha wanafunzi kuvaa mavazi watakavyo, tena kwa kanuni za mtaani wakati ni kigezo na nyenzo kuu ya utii na nidhamu, vilevile ndiyo utambulisho wake mkuu mwanafunzi.
Kanuni ya mvulana na msichana wanafunzi shuleni, wanavaa mashati yanayofanana, binti akiwa katika sketi na mvulana suruali, wote wanachomekea, soksi zinazofanana na aina ya vitatu maalum.
Je, wanatii? Ni ngumu hivi sasa kukuta wanafunzi wa shule moja wamevaa soksi zinazofanana, wamechomekea, wengine wakifika mbali kama kwenda shule na kandambili; mikasa ya wanafunzi kuvuta bangi ikishamiri.
Ni hali ya kawaida mitaa na miji mikubwa kama Dar es Salaam, ambako hadi saa mbili asubuhi wanafunzi wanazagaa mitaani.
Kwa mjumuiko huo, iwe mwanafunzi hata mwalimu wake kuna kasoro za nidhamu ya kazi, vyote vinaengua mwelekeo wa ufanisi darasani.
Hiyo ni kuanzia ngazi ya utii na nidhamu kwa pande zote, huku kukiwapo sumu ya tuisheni, inayoondoa ufanisi wa staili ya kuelewa ya asili kwa mwanafunzi.
· TUJADILI ZAIDI JUMANNE WIKI IJAYO.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED