Yanayokwaza mkakati kutokomeza VVU na UKIMWI yashughulikiwe

Nipashe
Published at 10:36 AM Dec 03 2024
Siku ya UKIMWI Duniani.
Picha:Mtandao
Siku ya UKIMWI Duniani.

KATIKA toleo letu la jana, tulikuwa na habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman wakija na mambo kadhaa ambayo ni kikwazo katika kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI kufikia mwaka 2030.

Akiwa mjini Songea, mkoani Ruvuma juzi, Dk. Mpango alitaja vikwazo hivyo vinajumuisha jamii kuwa na mtazamo hasi dhidi ya walioambukizwa virusi hivyo, hata kuchangia kurudisha nyuma jitihada za kupambana na UKIMWI.   

Mtazamo hasi, kama ilivyofafanuliwa na Makamu wa Rais, huwafanya wahitaji kushindwa kupata huduma kwa kuonekana kuwa hawastahili na hivyo kutengwa, huku akionya unyanyapaa husababisha woga unaoathiri upimaji kwa hiari na upatikanaji huduma nyingine kama za unasihi pamoja na ARV kwa wale wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU).  

Kuna angalizo lingine la Makamu wa Rais kwa vijana, kwamba wanapaswa kujitambua, kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa kasi ya maambukizi katika kundi hilo inaonekana kuwa kubwa. Takwimu za hali ya UKIMWI nchini zinaonesha kundi la vijana, hasa wa kike, liko katika hatari zaidi ya kupata maambukizi mapya ya VVU.  

Maambukizi mapya, kama ilivyoelezwa na Makamu wa Rais, yanachochewa zaidi na mazingira na tabia hatarishi hususan ulevi uliopindukia, ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi na matumizi ya dawa za kulevya.

 Matokeo ya utafiti  wa viashiria vya VVU na UKIMWI uliofanyika mwaka 2022/23, yanaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri kuanzia miaka 15 ni watu 60,000 kwa mwaka. Kiwango cha ushamiri wa VVU kitaifa ni asilimia 4.4 ambapo jumla ya watu 1,548,000 wanaishi na VVU. 

Ingawa kiwango cha ushamiri wa VVU kwa wenye umri kuanzia miaka 15 na zaidi kwa upande wa Zanzibar ni cha asilimia 0.4, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman, anataja changamoto zinazohusiana na haki za binadamu katika upatikanaji huduma za UKIMWI zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha juhudi za serikali na ulimwengu kwa ujumla katika kumaliza tatizo la UKIMWI.

 Akiwa mkoa wa Kusini Pemba juzi, Othman aliungana na Dk. Mpango kukemea unyanyapaa na watu kulazimishwa kupima, akionya kuwa hali hiyo husababisha watu kukosa na kuogopa kuzifikia huduma za kujikinga na VVU pamoja na za matibabu kwa wanaoishi na VVU. 

Othman pia alikosoa tabia ya baadhi ya mashirika na taasisi kuwalazimisha wafanyakazi wao hasa inapotokea haja ya kuongezwa mikataba, kupimwa kwa lazima, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za afya Zanzibar.

Nipashe, tukiwa wadau katika mapambano hayo, tunaungana na serikali na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhimiza kuwapo mikakati endelevu kuhakikisha kila mdau anashiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI, ikiwamo kuondoa unyanyapaa na kuhakikisha waliogundulika kuwa na maambukizi wanapatiwa matibabu. 

Pamoja na taarifa zilizotolewa hivi karibuni kuonesha kuna kushuka kwa maambukizi ya VVU nchini, Nipashe tunaona kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya janga hilo. Elimu kwa umma inapaswa kuendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali hasa ya vijana na wanawake ambao wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi.

Kwa kuwa kundi la vijana ambalo serikali imeweka wazi liko katika hatari zaidi, ni vyema wadau wa afya wakatilia mkazo zaidi kwa kuwaelimisha kuhusu hatari ya ugonjwa huo. Elimu inapaswa kutolewa katika shule, vyuo vya elimu ya juu, migodini na maeneo ya uvuvi ambako kuna hatari zaidi ya maambukizi kitaifa.

Vijana katika maeneo hayo wanakuwa hatarini kupata maambukizi kwa sababu ya kuwa na tamaa ya kupata vitu vizuri. Pia huko ndiko ambako watu wazima huwafuata na kuwashawishi kushiriki nao ngono zembe ambazo huchangia ongezeko la maambukizi ya VVU, 

Nguvu ya pamoja inahitajika katika kupambana na VVU na UKIMWI. Kama ilivyokuwa kaulimbiu wakati wa serikali ya awamu ya nne, Tanzania bila UKIMWI inawezekana. Kila mmoja achukue hatua.