KUNA baadhi ya mikoa nchini imekuwa ikitajwa kuongoza kwa kukithiri vitendo vya ukatili wa kijinsia, hususani kuanzia ngazi ya familia. Hiyo ni kutokana na jamii kuamini kuwa iko ndani ya mila na utamaduni wa makabila ya huko.
Mbaya zaidi, jamii hizo zimekuwa zikichukulia kuwa ni jambo la kawaida na kuamua kufanya siri kwa kuhofia wahusika, kuangukia kwenye mikono ya dola na kuchangia kuendelea kukithiri kwa matukio hayo nchini.
Kukithiri vitendo hivyo, sasa kumeziibua taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini kupinga, baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwapo jamii zisizo na elimu, kuhusiana na madhara ya vitendo hivyo. Wanaishia na hisia kwamba, hakuna haja ya kuyaripoti katika mamlaka husika.
Taasisi na mashirika hayo yamekuwa yakifanya kampeni hususani katika mikoa, ambako kumekithiri vitendo hivyo, kwa lengo la kuwaelimisha wananchi madhara yake na umuhimu wa kuripoti kwenye vyombo vya dola mahali panakotokea matukio hayo.
Kampeni hizo zimesaidia kuibua matukio mengi ya aina hiyo na mengine yaliyokuwa yakifanyika katika jamii, ingawa bado kwa uchache yapo yanayoendelea.
Vitendo hivyo ni pamoja na watoto wadogo kubakwa, kulawitiwa na kwa wanafunzi mabinti kukatisha masomo kwa kupata ujauzito wakiwa shuleni, huku wazazi wakiachiwa jukumu la kulea wajukuu.
Wengine wamekuwa wakikumbana na ndoa za utotoni, baada ya kulazimishwa kuolewa kutokana na tamaa za wazazi kupata utajiri wa haraka kupitia mahari, huku wakisahau kufanya hivyo ni kuwaharibia msingi wa maisha yao baadaye na hata kisheria wanawajibika.
Hali hiyo imekuwa ikichangia vitendo hivyo kuendelea kusambaa katika maeneo mengine nchini na hata kwenye taasisi za elimu kama shuleni, vyuoni na sehemu za kazi.
Hiyo ndio sababu ya viongozi wa taasisi, mashirika hayo na hata waliko serikalini, kupitia wizara husika, sasa wamesimama kidete kwa kuitaka jamii kubadilika na kuwafichua watu wanaojihusisha navyo.
Wakati ukanda wote wa dunia, ikiwamo Tanzania unaelekea kwenye Maandalizi ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambayo kila mwaka hufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10, jamii ibadilike na kuunga mkono jitihada hizo.
Jitihada hizo zifanyike kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, kwa sababu wanazidi kuharibu vizazi vya sasa na vijavyo.
Ushahidi unaonesha kwamba, vitendo hivyo vinaendelea kuota mizizi katika jamii, kutokana na baadhi ya vizazi kurithi kwa kushuhudia vinafanyika kuanzia katika umri wao mdogo.
Mfano wa matukio hayo ni yale ya kutisha ya mauaji yanayoendelea kutokea katika jamii, yakiwamo ya wanandoa na watoto wadogo wasiokuwa na hatia.
Kwa kufanya hivyo, niseme tutakuwa tunaelekea kuwa na taifa ambalo litafanikiwa kutokomeza matukio ya ubakaji wanawake na watoto, vipigo ambavyo vimekuwa vikisababisha wanawake kuuawa na wenzi wao na rushwa ya ngono vyuoni na sehemu za kazi.
Wakati hayo yote yakiendelea, utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (Tukielekea ‘Upingaji Ukatili Jinsia’, itukae vichwani, si vita lelemama), umebaini wasichana milioni 120 duniani walilazimishwa kufanya ngono bila ya ridhaa yao.
Nao wanawake na wasichana milioni 200 walifanyiwa hayo ya ukeketaji katika nchi 30 duniani, huku wasichana na wavulana milioni 246 wakikumbana na ukatili wa kijinsia wakiwa shuleni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED