WATANZANIA leo wanaungana na watu wa mataifa mengine duniani kusherehekea Mwaka Mpya wa 2025. Kwa ujumla, furaha hiyo inatokana na ukweli kwamba kwa neema ya Mungu, wamevuka mwaka 2024 salama salmini kwa kuwa wako ambao walianza nao mwaka lakini wametangulia mbele za haki.
Katika kusherehekea Mwaka Mpya, baadhi ya watu husherehekea kwa kufanya ibada ikiwa sehemu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea kwa mwaka mzima ikiwamo kuwapa neema ya kuvuka mwaka uliopita na kuingia mwaka mwingine.
Baadhi ya watu, katika kuaga na kuukaribiha Mwaka Mpya, wanafanya tathmini ya malengo waliyoyaweka mwaka uliopita ili kuona wamefanikiwa kwa kiasi gani na kwa baadhi ya mambo kuona ni vikwazo gani vilivyosababisha wasifikie matarajio yao na hatimaye kupanga mipango mipya kwa mwaka unaofuata.
Wakati hayo yakifanyika, watu katika medani za kijamii, kisiasa na kiuchumi, huangalia kwa kina, urefu na mapana mambo yaliyojitokeza mwaka uliopita na kujaribu kutoa ushauri nini kifanyike. Kama ni wanasiasa, wanajaribu kutathmini matukio makubwa yaliyotokea katika medani hiyo.
Mwaka 2024 kwa mfano, katika siasa, imeshuhudiwa kuwapo kwa mambo mbalimbali ukiwamo uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ulifanyika Novemba na kuwapo kwa malalamiko mengi kwamba haukuwa huru na wa haki. Malalamiko hayo yalitolewa zaidi na wapinzani na wanaharakati waliosema mambo yaliyojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2019 yalijirudia tena na kusababisha hali hiyo.
Jambo lingine lililojitokeza na kupigiwa kelele na baadhi ya wanasiasa, viongozi wa dini na wanaharakati wa haki za binadamu ni matukio ya utekaji na mauaji na watu wengine kukamatwa na kupotea kusikojulikana. Lawama kubwa katika hilo pia zilielekezwa kwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.
Huku hayo serikali ikitupiwa mzigo wa lawama, jinamizi la ajali za barabarani zilitikisa nchi nzima na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha na wengine wapata ulemavu wa kudumu wa viongo. Sababu kubwa kuhusu ajali hizo ni uzembe wa madereva kwa kushindwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Kama wahenga wasemavyo hakuna jambo lisilokuwa na sababu, ni vyema kasoro hizo zilizojitokeza kwa mwaka 2024 kama vile uchaguzi kutokuwa huru na haki, watu kutekwa, kukamatwa na kuuawa na ajali za barabarani, ni vyema kila mtu, taasisi na serikali zilizopewa kazi ya kusimamia majukumu husika, zikasimamia haki na hatimaye iondokane na lawama katika masuala husika.
Mwaka 2025 kunatarajiwa kufanyika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa Tanzania pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Ni vyema Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zikahakikisha mchakato huo unafanyika kwa misingi ya uwazi bila upendeleo ili uwe huru na wa haki. Kwa maneno mengine, tume hizo zitangaze matokeo halisi ya uchaguzi badala ya chama fulani.
Kwa masuala ya watu kutekwa na wengine kuuawa, ni vyema serikali ikaimarisha ulinzi na usalama na pale panapotokea mauaji, uchunguzi ufanyike na wanaobainika au kutuhumiwa kuhusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Kuhusu ajali za barabarani, kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kukomeshwa kwa matukio hayo, Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, likachukua hatua madhubuti kukomesha matukio hayo. Kama ni ubovu wa magari, ni vyema yakazuiwa kufanya safari ili kuokoa maisha ya watu.
Iwapo kila mmoja atasimama kikamilifu katika nafasi yake, ni dhahiri kwamba amani, upendo, umoja na mshikamano vinavyoimbwa kila siku vitashamiri na Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Mwaka mpya wa 2025 uwe wa amani na upendo kwa Watanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED