Hongera TFF kuipeperusha Tanzania kibabe CAF 2024

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:34 AM Dec 28 2024
Hongera TFF kuipeperusha  Tanzania kibabe CAF 2024
Picha:Mtandao
Hongera TFF kuipeperusha Tanzania kibabe CAF 2024

ZIMESALIA siku tatu tu kumaliza mwaka 2024 na haitarejea tena kwenye dunia hii, ila utabaki kwenye kumbukumbu.

Katika rekodi ambazo zitawekwa ni  umekuwa mwaka wa mafanikio makubwa katika medani za michezo hasa kwenye soka.

Kwanza kabisa, tunaanza kwa klabu mbili za Tanzania, Simba na Yanga kutinga  hatua za makundi ya michuano ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Yanga imetinga hatua ya makundi kwenye Ligi Mabingwa Afrika, huku Simba ikiwa ndani iachuana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa miaka ya hivi karibuni imeonekana ni kawaida kwa timu za Tanzania, hasa Simba ambayo imeingia mara nyingi zaidi na sasa Yanga imeanza taratibu kuzoea kuingia hatua hiyo.

Ukiacha hilo, mwaka 2024 umeonekana kutia fora kwenye timu za taifa za soka, timu saba zimefanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika.

Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, ndio ilikamilisha idadi ya timu za Tanzania zitakazokwenda kucheza fainali za AFCON U-17, zitakazofanyika nchini Morocco mwakani.

Hii ni baada ya kuichapa, Sudan Kusini mabao 4-0, katika mchezo wa nusu fainali katika michuano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Tanzania pia mwaka huu ilifuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa walemavu (BAFCON), yaliyofanyika mwaka huu nchini Misri.

Kikosi cha timu ya taifa chini ya miaka 15 nacho lilifanikiwa kufuzu fainali za mashule barani Afrika, huku Tanzania ikiwa mwenyeji.

Timu ya taifa chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes)nayo haikuwa nyuma, kwani ilifuzu fainali za AFCON, ambazo zinatarajiwa kufanyika Ivory Coast.

Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars nacho waka huu kilifanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika (WAFCON), zinazotarajiwa kuchezwa Morocco.

Kama vile haitoshi Tanzania imepeleka fainali timu mbili za soka wanaume, moja ya wachezaji wa ndani ya nchi na nyingine ni ya jumla.

CHAN, michuano ya wachezaji wa ndani, Stars ilifuzu fainali hizo zinazotarajiwa kupigwa mwakani katika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.

Taifa Stars, timu kubwa ya soka Tanzania yenye wachezaji wote wa ndani na nje, imefanikiwa kufuzu (AFCON), zinazotarajiwa kuchezwa Morocco pia.

Kwa hili hatuwezi kupita bila kulipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), chini ya uongozi wa, Rais Wallace Karia.

Uongozi wa Karia umeonekana kujipambanua si tu kuibua vipaji vya soka la vijana wanaume na wanawake, lakini pia kutengeneza vikosi imara vya kila timu ya taifa na umri wake, zinazokwenda kuleta ushindani kubwa barani Afrika. Nadhani umekuwa na mpango mkakati sahihi na wakati sahihi, pamoja na kuchukua vijana wenye umri sahihi na vipaji sahihi pia.

Ni uongozi ambao umekuwa ukiamini mchezaji mwenyewe kupambana kwa uwezo wake na si kuwekeana kanuni za wazawa kupata upendeleo wa kucheza na kuzuia wageni.

Hii imefanya pia wachezaji wa Kitanzania kuanza kupambana bila kutegemea mbeleko ya uzawa.

Hivi karibuni nilimsikia akikataa uashauri wa baadhi ya wacheambuzi kuwepo kwa kanuni ya makipa watupu wa kizawa, akiwaambia hata wao wazawa wanahitaji makipa wageni ili na wao wajiboreshe na kwa maana hiyo Tanzania itapata makipa wazuri.

Akasema hawezi kuipangia timu kumweka kipa mzawa, badala yake makipa wote wanatakiwa kuonyesha ushindani na makocha wapange bila kujali ni Mtanzania au mgeni, badala yake kiwango ndicho kitaamua.

Na hii ni baada ya pia mwanzoni mwa msimu baadhi ya wadau kutaka kupunguzwa kwa wachezaji 12 wa kigeni wanaohitajika kikanuni, lakini kiongozi huyo na baadhi ya wadai walipinga kwa madai watapunguza msisimko wa ligi, kwani moja ya vitu vinavyoifanya Ligi Kuu Tanzania kuvutia ni kuwepo kwa wachezaji mbalimbali kutoka bara la Afrika, na hata mabara mengine duniani.

Karia na TFF yake inastahili pongezi kwa kuongoza kwa kutofuata mihemko ya mashabiki na wachambuzi, matokeo yake Tanzania imekuwa ikipiga hatua.

Hongera TFF, ni nyinyi mlioipa sifa Tanzania kumaliza mwaka 2024 kwa kishindo, timu zake saba kufuzu michuano ya CAF ambayo miaka ya nyuma wadau na mashabiki wa soka walikuwa watazamaji tu.