VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga zote za Dar es Salaam ndio timu wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wao wanashiriki hatua ya makundi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati, Simba 'Mnyama' wenyewe wanapeperusha bendera ya Tanzania katika hatua hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga iliyoko Kundi A inaburuza mkia baada ya kuvuna pointi moja baada ya kucheza mechi tatu za hatua ya makundi, na leo itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuwakaribisha TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).
Mechi ya leo kwa Yanga ni muhimu sana kwa sababu inahitaji kuzibakisha pointi zote tatu ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka, matokeo chanya pekee ndio yatawafanya warejeshe nguvu ya kupambana kwenye michezo iliyobakia ya hatua hiyo ya makundi.
Endapo Yanga itapata ushindi, mechi zake mbili zitakazobakia pia zitakuwa ni za maamuzi na si za kucheza ili kukamilisha ratiba kutoka kwa Al Hilal ya Sudan yenye pointi tisa, tayari kuweka mguu mmoja ndani katika hatua ya robo fainali.
Na kwa upande wa Simba ambayo pia iko Kundi A, na kwenye msimamo iko katika nafasi ya tatu, ikiwa na pointi sita sawa na Bravos do Maquis ya Angola na CS Constantine, zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, inahitaji ushindi ili kujiimarisha kwenye msimamo wa kundi hilo.
Simba itakuwa ugenini, hilo si tatizo kwa sababu endapo watacheza karata zao vyema, basi wanaweza kupata ushindi au kuambulia sare, kikubwa ni wachezaji kujituma, kuongeza umakini na kutowadharau wapinzani wao kwa kuangalia matokeo ya mchezo uliopita.
Haijalishi Mnyama kesho anacheza ugenini, tena kwenye ardhi ya Mwarabu, katika mpira lolote linaweza kutokea kama wachezaji wataingia kwa kuuona mchezo huo ni wa fainali na wanachotakiwa kukifanya ni kushinda ili kurejea na kikombe nyumbani.
Kufanya vizuri kwa vigogo hao, sio tu kutaipa heshima Tanzania, lakini wataendelea kujihakikisha kutoa wawakilishi wanne katika mashindano yajayo ya CAF, kama Algeria, Misri na Morocco ambao hiyo imekuwa ni kawaida kwao.
Ili kuhakikisha wanajipanga vyema, bado makocha wanayo nafasi ya kuimarisha vikosi vyao kwa kufanya usajili ambao utawafikisha kwenye malengo yao, klabu zinatakiwa kutumia dirisha hili la usajili kuwanasa nyota wanaoendana na hatua ambazo wanataka kufika.
Tunawakumbusha viongozi wa Simba na Yanga kuacha kusajili wachezaji ambao wanahitaji kupata muda ili wawe wazoefu, ongezeni 'silaha' ambazo ziko tayari kuingia katika mapambano, isiwe wanaangalia washindani wao katika Ligi Kuu Tanzania Bara pekee, wasajili wachezaji wenye uwezo wa kuhimili mikikimiki dhidi ya klabu nyingine kongwe za Afrika.
Umefika wakati wa Simba na Yanga sasa kuweka malengo ya kutwaa taji la Afrika la Kombe la Shirikisho au Ligi ya Mabingwa na si kupambana kucheza robo fainali au nusu fainali. Ndoto kubwa ya mashabiki na wadau wa michezo nchini ni kushuhudia moja ya taji hilo la CAF linatua katika ardhi ya Tanzania.
Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha wachezaji wa Simba na Yanga kuwakabili wapinzani wao kwa tahadhari na kutowadharau, wakumbuke hakuna timu iliyofika hatua ya makundi inahitaji kusindikiza wengine, kila timu inahitaji kuweka historia.
Kusonga mbele katika mashindano hayo mawili, sio tu kutalitangaza vyema jina la Tanzania kimataifa, lakini itaendelea kumpa heshima Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa shabiki namba moja wa michezo nchini.
Kwa hapa nyumbani, huu ni wakati muhimu wa mashabiki wa soka bila kujali itikadi, kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia Yanga, shabiki ni mchezaji wa 12, kama ambavyo tunashuhudia mechi za dabi zinajaa au Tamasha la Wiki ya Mwananchi, leo ni siku nyingine muhimu kwenda kuwapa hamasa wachezaji ili kupata pointi tatu.
Mungu ibariki Simba na Yanga, katika vita ya kusaka tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF katika ngazi ya klabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED