Tunakutakia 2025 yenye mafanikio

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 08:52 AM Jan 01 2025
Tunakutakia 2025  yenye mafanikio
Picha:Mtandao
Tunakutakia 2025 yenye mafanikio

LEO Watanzania kote walipo majijini, mijini na vijijini wanakusanyika pamoja na familia na marafiki kuushangilia mwaka mpya.

Nipashe Mwanga wa Jamii inawataka wasomaji na watangazaji wetu  na kila mtu heri ya mwaka mpya 2025.

Heri zetu zinaambatana na kuwatakia afya tele, furaha na mbinu mpya za utafutaji ili kuwa na maisha bora zaidi.

Huu daima ni wakati wa matumaini, tunapoadhimisha mwisho wa mwaka mmoja na mwanzo wa mwingine tuna matumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri au sawa.

 Na ingawa mwaka wa 2024 kwa wengine ulikuwa mgumu kwa gharama  za maisha kuzidi kuongezeka, upatikanaji wa pesa pia kuwa mgumu  na ughali wa chakula nao ni changamoto. Hilo halituyumbishi, tuna matumaini. 

Hata hivyo, lazima pia tuangalie nyuma, tukiamini kuwa mwaka huu unaleta siku angavu zaidi  tena ziko mbele yetu na  kwamba ingawa changamoto zetu ni kubwa, kila mmoja wetu ana ujasiri na dhamira ya kuisimama  na kukabiliana nazo 2025.

 Ni roho hiyo ambayo imezifanya familia zetu na taifa kuwa hai na ni roho hiyo ambayo itaiweka hai nchi hii na sisi raia wake kwa vizazi vijavyo.  

Wakati huu, tunatafakari juu ya nguvu inayotuweka pamoja kama raia na taifa letu la Tanzania.

 Tunaitazama michango ya serikali kwa maendeleo yetu na sisi pia tuangalie michango yetu kwa maendeleo ya familia zetu na nchi pia. 

Tujue kuwa huu ni wakati wa kujikumbusha kwamba kila mtu ni mchezaji kwa mafanikio ya nchi yetu. Si jukumu la serikali pekee na sisi pia.

Sisi ni taifa tajiri lenye rasilimali nyingi tuazimie tufanye kazi kwa uaminifu na uaminifu kwenye ngazi zote nyumbani, viwandani, ofisini, shambani na hata kwenye viwanja vya mpira na majukwaa ya burudani tubadilishe maisha yetu.

Ni lazima pia tujue kuwa tuna  tamaduni na mila tofauti tunahitaji kuvumiliana  na kushirikiana  kujenga nchi yetu ili taifa liwe  bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo. 

Ni lazima kutii sheria kuanzia za barabarani, za ardhi za elimu, kilimo na pia kupenda kutafuta taarifa sahihi ili tupate ufahamu na maendeleo. 

Kupitia bidii, umoja, juhudi na uvumilivu  na umoja Watanzania tushirikiane kuendeleza rasilimali na ujasiriamali, umiliki wa biashara na kuwa na fikra za kubadilika kuendeleza taifa bila kutegemea misaada na uhisani.

Kila mmoja ajengwe na imani kwamba Tanzania ni yetu na katika nchi hii kubwa yenye karibu watu milioni 65 na utajiri mwingi, yeyote anaweza kuifanya ikiwa bora zaidi hivyo ajaribu.  

Aidha, kila mmoja awe kuwa mwaminifu kujenga taifa, kutunza fedha za umma, kusimamia na kujenga miradi bora kama shule, hospitali, miundombinu na mingine mingi ili kuwa na Tanzania bora zaidi.

 Ndiyo maana ni muhimu zaidi kuliko mwaka jana kwamba tutajirekebisha ili  kuwa na mawazo chanya na kupaza sauti zetu na kutumia fursa zilizopo kufikia maendeleo kwa wote.

Iwe unasherehekea mwaka wa 2025 ukiwa kazini, au bila kuwa na ajira, makazi bora au hata kama unaumwa kuwa na matumaini  kwamba sote tunaweza kutafuta na kupata  fursa na mafanikio. 

Tunaweza kuibadilisha Tanzania sisi wenyewe siyo lazima awepo wa kutusaidia. Kwa hiyo mabadiliko yaanze na wewe.

 Fikiria kuwa katika kufikia maendeleo mpe Mungu asilimia 75 na wewe ujibakizie asilimia 25.

Katika kufanya hivyo hutahangaika na ushirikina na kuwaua watoto, wanawake na wenye ulemavu. Utaacha uhalifu, utakuwa na hofu ya Mungu, hutaiba mali wala fedha za umma wala za watu kupitia mikataba au udanganyifu wowote.

Kadhalika kunyanyasa wengine kingono, utaacha uongo wala hutatamani mali za dhuluma na lolote linalokuingiza kwenye hatia.

Nipashe inakutakia wewe na wapendwa wako furaha, ustawi, afya njema na bahati  katika mwaka mpya wa 2025.

Heri ya Mwaka Mpya, kila mtu.