ASANTE Mungu, ndio neno tunalostahili kusema Watanzania na hasa mashabiki na wadau wa mpira wa miguu hapa nchini kutokana na mafanikio ambayo timu zetu zimepata.
Baada ya kumshukuru Mungu, ni wakati mwingine wa kuwapongeza viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), walioko chini ya Rais, Wallace Karia kwa kuongoza timu zake kufanya vyema katika mechi za kusaka tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya CAF.
Inajulikana wazi, jitihada hizi hazikuwa za TFF peke yake, Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan, ilikuwa karibu katika kuhakikisha mafanikio hayo yanapatikana na Watanzania wanapita kifua mbele dhidi ya wapinzani wao.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania imekata tiketi ya kushiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa timu zake saba, na zimefanya hivyo katika kipindi cha mwaka 2024, ambao umebakiza siku chache ili kumalizika.
Timu saba za Tanzania zitapeperusha bendera ya nchi katika fainali tofauti, na fainali hizo zote zikitarajiwa kuchezwa mwakani.
Timu ya kwanza ni ile ya soka (Taifa Stars), ambayo itashiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), huko nchini Morocco, timu hii ilifuzu kibabe baada ya kuchukua pointi tatu za ugenini dhidi ya Guinea, na ikazibeba za nyumbani katika mchezo wake wa mwisho.
Wawakilishi wengine wa Tanzania watakaoshiriki mashindano ya Afrika ni kikosi chenye wachezaji wanaocheza ligi za ndani na fainali zao maarufu hujulikana kwa jina la CHAN, fainali hizi zitafanyika hapa nyumbani na hii ni sehemu ya maandalizi ya kuwa wenyeji wa fainali za mwaka 2027.
Twiga Stars, Timu ya Taifa ya Wanawake, pia imefuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, awali fainali hizi zilitarajiwa kuchezwa mwaka huu huko Morocco, lakini kwa sababu ambazo ziko nje ya CAF, zilisogezwa mbele na sasa zitafanyika kuanzia Julai 6 hadi 26, mwakani.
Vijana wenye umri chini ya miaka 20 maarufu Ngorongoro Heroes pia wamefuzu kushiriki fainali za AFCON U-20, Serengeti Boys wamekata tiketi ya kwenda kuwania taji la Afrika la AFCON U-17 pamoja na wadogo zao U-15 ambao watakwenda kupambana kwenye michuano ya Shule ya Afrika.
Kufuzu ni jambo moja, lakini kufanya vizuri katika mashindano hayo ni jambo lingine. Ili timu zetu ziende katika fainali hizo bila wasiwasi, zikijiamini na zikiwa na morali, ni lazima zipate maandalizi mazuri na maandalizi hayo yafanyike mapema.
Huu ni wakati wa Serikali na viongozi wa TFF kuanza mapema maandalizi kwa sababu ile ahadi ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA' ya kutaka kuweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa CHAN na kuvuka hatua ya makundi kwenye fainali za AFCON 2025 inatimia, basi ni kuanza kuziandaa timu hizi mapema.
Maandalizi ya zimamoto kamwe hayatatusaidia Watanzania, bado tusiamini wachezaji wetu wanaweza kuwa tayari kwa mashindano kwa kuwaweka pamoja siku chache kama wanavyofanya wenzetu ambao vikosi vyao vinaundwa na asilimia kubwa ya nyota wanaosakata kandanda la kulipwa Ulaya.
Hata ikiwezekana ligi kusimama, huu ndio wakati ambao hatutakiwi kukosea, tunatakiwa tuwe na mikakati ya kubeba ubingwa na kumrejeshea furaha Rais Samia ambaye amekuwa shabiki na mdau namba moja wa michezo hapa nchini.
Wakati Serikali ya Tanzania ikijipanga kuziandaa vyema timu, wachezaji watakaopata nafasi ya kuitwa katika timu hizo wanatakiwa kufahamu hiyo ni fursa yao kubwa ya kujiweka sokoni kwa kupandisha thamani zao.
Mashindano ya AFCON yamekuwa ni daraja kwa wachezaji wa Afrika kuonekana na makocha wa Ulaya, hivyo nyota wetu wajiandae kucheza kwa juhudi ili kuipa nchi matokeo chanya na vile vile kujitafutia soko katika timu za nje.
Tunapenda pia kuwapongeza makocha wazawa wakiongozwa na Hemed Suleiman 'Morocco' kwa kuzifundisha timu zetu na kuufanya mwaka 2024 kuwa wa kihistoria katika upande wa soka hapa Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED