Mapinduzi Cup iwe chachu ya kupata 'silaha' za CHAN

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:49 AM Jan 04 2025
Mapinduzi Cup iwe chachu  ya kupata 'silaha' za CHAN
Picha: Mtandao
Mapinduzi Cup iwe chachu ya kupata 'silaha' za CHAN

MASHINDANO ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu yameanza kufanyika kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, Zanzibar jana kwa 'wanandugu' Timu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), ilipowakaribisha Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars).

Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa Timu ya Taifa ya Burkina Faso itakapocheza dhidi ya Harambee Stars ya Kenya, michezo yote ikipigwa, saa 20:15, usiku.

Fainali ya michuano hiyo itafanyika Januari 13, mwaka huu kwenye uwanja huo huo wa Gombani.

Kumekuwa na tofauti kidogo kwenye michuano hiyo msimu huu. Badala ya klabu kuchuana, sasa imezishirikisha timu za taifa.

Sababu inaeleweka. Kumekuwa na mwingiliano wa ratiba hasa kwa timu za Simba na Yanga ambazo ni washiriki 'wakubwa' wa michuano hiyo, wamebanwa na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikumbwe michuano ya kimataifa imeanza mapema sana msimu huu kutokana na ifikapo Februari, mwaka huu kuna Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazopigwa hapa nchini, Kenya na Uganda.

Pamoja na mengine, waandaaji wa michuano hiyo wakaona wabadilishe mfumo, badala ya timu za klabu basi zicheze timu za taifa.

Timu zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo ni nne, wenyeji Zanzibar, Tanzania Bara, Burkina Faso na Kenya, ambazo tayari zipo visiwani kwa ajili ya kuanza kupambana kuwania kombe hilo.

Tunaipongeza kamati ya maandalizi ambayo haikuona sababu yoyote ya kuahirishwa michuano hiyo licha ya changamoto zote hizo.

Tumeona wachezaji waliochaguliwa kwa pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar wengi wao ni vijana ambao bado wana safari ndefu katika soka la nchi hii.

Kamati ya Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) na Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ahmad Ally, amejitahidi sana kuchagua wachezaji vijana kutoka Serengeti Boys (U-17), Ngorongoro Heroes (U-20),  pamoja na wale ambao waliokuwa wanaitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars lakini hawapati namba.

Wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza mbele ya wachezaji kama Mbwana Samatta, Simon Msuva na baadhi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.

Ukiacha wachezaji wa Simba, Yanga na Azam, ambao baadhi yao wanaitwa ama kwa mazoea, au viwango wanavyoonyesha kwenye Ligi Kuu na michuano ya kimataifa, michuano hii itasaidia mno kutazama wachezaji kutoka timu nyingine ambazo wamekuwa hawaonekani au kutazamwa sana na mashabiki.

Bara na Zanzibar kwa sasa zina wachezaji ambao hawatokani na Simba na Yanga, hivyo ni fursa sasa ya wachezaji wenyewe kuonyesha walichonacho ili kuondoa dhana timu hizo ndizo zinazotoa nyota wenye ubora.

Tumeona kuna wachezaji wengi kutoka timu za Ligi Kuu Bara, na Zanzibar, sasa hii ni fursa kwao kwa sababu ni jukwaa la kuteuliwa kuunda kikosi cha CHAN.

Kocha Ahmed, amekiri mchezaji  atakayefanya vyema katika michuano hii, ana uwezekano mkubwa wa kuwamo katika kikosi cha CHAN ambacho nadhani kitatajwa hivi karibuni.

Wakipatikana kutoka Zanzibar, halafu wengine Bara, na baadhi waje kuongezwa kutoka Simba na Yanga, nadhani tunaweza kupata kikosi bora.

Hata hivyo ni lazima kwanza wachezaji wenyewe walioitwa kufanya kazi ambayo kila mmoja ataona ni kweli wanastahili kuitwa.

Bahati nzuri kwenye vikosi vyote hivi viwili, hakuna wachezaji kutoka nje ya nchi, wala Simba na Yanga, hivyo hakuna visingizio, kazi kwao.