Mwaka 2025 ukuweke mama mbali na kashfa uvutaji bangi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:06 PM Jan 02 2025
Uvutaji bangi.
Picha:Mtandao
Uvutaji bangi.

MWAKA uliopita ulibainika kuwa na ongezeko kubwa la wanawake wanaovuta bangi, ikidaiwa lengo lao ni kuwapunguzia msongo wa mawazo.

Mbali na lengo hilo, wengine walijihusisha na uvutaji bangi, kutokana na migogoro ya kimapenzi, pia kutumia kilevi hicho kama starehe, pasipo kujali madhara yake kiafya.

Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, akiwasilisha taarifa ya operesheni ya kusaka dawa za kulevya iliyofanyika nchi nzima kati ya Oktoba na Novemba mwaka jana.

Anataja bangi aina ya 'skanka' inayosemekana kuwa na kiwango kikubwa cha sumu kali, lakini wanawake ndio wanaitumia bila ya hofu.

Nimegusia kidogo hali ilivyokuwa mwaka jana, ili kuwakumbusha wanawake kuwa tunapoanza mwaka mpya wa 2025, tutambue madhara ya kilevi hicho na umuhimu wa kuachana nacho.

Tuingie mwaka mpya na mambo mapya hasa kwa kuanza maisha mengine yasiyogusa bangi ili kulinda afya, kwani wataalamu wa afya wanasema uvutaji huo, husababisha madhara makubwa katika mapafu ya mvutaji. 

Vilevile kuna kero ya kama kukohoa na koo kuwasha na kwamba, uvutaji huo wa bangi unamweka mvutaji katika hatari mara tano zaidi ya kupata saratani ukilinganisha na mvutaji sigara.

Pia, kuna haja ya kusonga mbali zaidi kuwa, licha tu ya matatizo ya ubongo yanayoathiri afya ya akili kwa mvutaji, bado inaangukia kundi kwamba, ni ugonjwa mbaya unaowapata wavutaji bangi.

Kwa kifupi, anayevuta bangi huwa na uwezo mdogo wa kumbukumbu. Uvutaji wa hizo dawa za kulevya, humwondolea mtu uwezo wa asili wa kufanya maamuzi sahihi, akilinganishwa na mtu asiyejihusisha na matumizi ya bangi.

Hivyo, ili kuondokana na madhara hayo, ni vyema kutojihusisha na uvutaji wa dawa hizo zenye madhara makubwa kiafya.

‘Ukiwa bado ni mbichi’ tukitumia lugha ya mtaani, ni kwamba mwaka 2025 uwe ni watu kuwa huru, kutoka katika kifungo cha matumizi ya bangi.

Ni kwamba, mtumiaji anapovuta msokoto huo, anaanza kufanya kazi baada ya dakika chache na yeye huanza kuhisi mapigo ya moyo yakienda mbio.

Kwa kuwa mvutaji, pia huanza kubadilika na kuona vitu visivyo katika uhalisia kutokana na maruweruwe: Matokeo ya muda mfupi baada ya kuvuta moshi, basi wale wote wanaojihusisha na wengine wanaotamani, ni vyema wakaacha.

Wanaitumia dawa hizo za kulevya kama njia ya kuondoa msongo wa mawazo, wakumbuke kuwa wanahatarisha afya zao.

Kwanini tuendekeze mabaya haya, dhidi ya tija zetu kiafya? Kwa watu wenye msongo wa mawazo au migogoro ya kimapenzi, jambo jema kwao ni kuwaona washauri nasaha au wataalamu wa saikolojia. 

Hatua hiyo ije na mapya yake, iwe ya kuweka sawa kwa ajili ya kulinda afya zao badala ya kuziangamiza kama njia ya kupata unafuu katika migogoro.

Ninaamini kwamba anaweza kuwaweka sawa watu wenye matatizo hayo, sio kutegemea dawa za kulevya, ambazo kimsingi ni hatari kwa watumiaji na pia zinaweza kuwaweka matatani pale wanapobainika kujihusisha.

Vilevile, wanaotumia bangi kama starehe, ni vyema nao wakatumia vitu ambavyo havina madhara kiafya, kwa sababu kuvuta dawa hizo sio starehe bali ni kujiangamiza bila kujua.