Wanaokopa taasisi zisizo rasmi zingatieni ushauri wa BoT

Nipashe
Published at 12:02 PM Jan 02 2025
Majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Picha:Mtandao
Majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

KUMEKUWA na vilio na malalamiko huku baadhi ya watu kufikia hatua ya kupoteza maisha kutokana na kujiingiza kwenye mikopo ambayo inatolewa na taasisi zisizo rasmi.

Baadhi ya wananchi huingia kwenye mikopo hiyo kwa kushawishiwa na taasisi hizo kwa maneno matamu ili kuvutia wateja kukopa huku lengo lao likiwa kuwakamua wakopaji hao.

Kuna wanaoingia kwenye mikopo hiyo kwa kutafuta njia rahisi ya kupata fedha kwa haraka badala ya kufuata njia sahihi zinazotolewa na benki zinazotambulika.

Matokeo yake ni wakopaji hao kudhalilishwa kwa kunyang’anywa samani zao na wengine nyumba zao kupigwa mnada na baadhi kutokana na udhalilishaji huo hupata msongo wa mawazo na kujitoa uhai.

Kinamama ni waathirika wakubwa wa mikopo hiyo kutokana na shughuli zao za ujasiriamali wakitaka kuongeza mitaji kwa kujaribu kukopa, lakini huishia kufilisiwa mali zao.

Viongozi mbalimbali wa kisiasa kila mara wanatoa tahadhari wananchi kujiepusha na mikopo hiyo ambayo kwa jina maarufu hujulikana kama ‘mikopo umiza’, lakini kama wahenga wanavyosema sikio la kufa halisikii dawa. 

Ili kuwaepusha wananchi na kadhia hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepiga marufuku taasisi zinazojishughulisha na utoaji wa mikopo bila kuwa na leseni inayotambulika kisheria.

BoT imetoa marufuku hiyo baada ya kubainika uwapo wa baadhi ya taasisi zinazotoa huduma ya kifedha hususani ya mikopo bila ya kutambulika kisheria kuendelea kutoa huduma hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, huduma hizo za kifedha zinatakiwa zitolewe na taasisi ambazo tayari zimepewa leseni ya kufanya kazi hiyo.

Kwa mujibu Tutuba, Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, ni kosa kwa taasisi, kampuni na watu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Aidha, Kifungu cha 16(2)(a) cha sheria hiyo kimeainisha adhabu inayopaswa kutolewa kwa kuendesha biashara ya kukopesha bila kuwa na leseni ikiwa ni pamoja na kutozwa faini isiyopungua Sh.milioni 20 au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili au vyote kwa pamoja.

“Hivyo basi, Benki Kuu inapenda kuusisitiza umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye hana leseni.”

“Endapo taasisi au mtu binafsi anataka kufanya biashara ya ukopeshaji, anatakiwa kufuata taratibu husika za kuomba leseni kutoka BoT ili apewe kwa mujibu wa sheria. Ni muhimu mtu anapotaka kukopa, atumie taasisi zenye leseni ya BoT ili kuhakikisha kuwa huduma anayopata ni salama na inayozingatia sheria za nchi.”

Benki hiyo pia imeshangazwa na uwapo wa taarifa katika mitandao ya kijamii zinazohusisha alama za wanyama kama vile kobe na nyoka katika utoaji wa mikopo na kwamba jambo hilo ni kinyume cha sheria na maadili ya utoaji huduma za kifedha.

“Wananchi wanashauriwa kupuuza taarifa hizo na kutokujihusisha nazo kwa kuwa hazijapewa leseni hapa nchini.”

Wananchi kama wanataka huduma hiyo ya kifedha, wameshauriwa watumie taasisi zenye leseni za kukopesha zilizoidhinishwa na BoT pamoja na zenye leseni za mikopo ya kidijitali ambazo zipo kwenye tovuti ya benki hiyo.