MWANZONI mwa mwaka huu, Tanzania ilikuwa na uhaba wa walimu 39,610 wa masomo ya sayansi na hisabati ambao ni sawa na asilimia 55.8.
Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba.
Ni taarifa anayoitoa bungeni jijini Dodoma akijibu swali la mmoja wa wabunge aliyetaka kujua nchi ina upungufu wa walimu kiasi gani wa shule za msingi na sekondari kwa masomo ya sayansi na hisabati.
Wakati kukiwa na mazingira hayo, baadhi ya wazazi na walezi wamebuni mbinu za kukabiliana na changamoto hiyo ambazo ni kuwalipa posho walimu wa kujitolea ili wazibe pengo hilo kwa muda.
Hayo yanafanyika kwenye baadhi ya shule, huku serikali ikiendelea na mchakato wa kuajiri walimu wapya kumaliza au kupunguza uhaba wa walimu katika shule za umma hasa sekondari.
Kuna maeneo wazazi na walezi wameamua kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo, kwa kuwalipa posho walimu wa kujitolea ili kusaidia kuinua kiwango cha elimu katika sekondari hizo.
Viwango vya malipo vinatofautiana wakiwamo ambao kila mmoja analipa Sh. 1,000 kwa mwezi huku wengine Shilingi 900 kwa mwezi, ili kuhakikisha watoto wao wanafundishwa masomo yote wawapo shuleni.
Juhudi za wazazi na walezi hao hazijaishia katika kulipa posho za walimu wa kujitolea tu, bali pia wanashiriki kwa hali na mali kujenga sekondari mpya zikiwamo za vijiji na kata mpya na pia vyumba vya madarasa kwa zile zenye upungufu.
Hatua hiyo inaonyesha jinsi ambavyo wanatambua kuwa shule hizo ni mali yao, wana wajibu wa kuzihudumia pale inapowezekana kwa kuboresha kiwango cha elimu kwa watoto wao.
Aidha, hatua hiyo inaonyesha ni jinsi gani wazazi na walezi wanashirikishwa kwa kupewa taarifa sahihi na kuhamasishwa kwa ajili ya maendeleo ya shule zao na hivyo kuwafanya wawe tayari kuzihudumia.
Shule za serikali ni za umma, ambao ni wananchi, hivyo wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kuajiri walimu zaidi, ni muhimu umma ukabuni mbinu za kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao.
Mfano huo wa kutoa posho kwa walimu wa kujitolea ni wa kuigwa na wazazi na walezi kote nchini, kwa kuwa una mchango mkubwa kwenye maendeleo ya elimu kuliko kukaa pembeni na kudhani hawahusiki.
Ikumbukwe kuwa watoto wengi nchini, wanasoma shule za umma, ambazo zinatajwa kuwa uhaba wa walimu, hivyo ni wajibu wa umma kuzihudumia kadri inavyowezekana, ili ziwe na maendeleo mazuri.
Wazazi na wazazi wanaoishi vijijini ambako shule za huko zinadaiwa kuwa na uhaba wa walimu, ni vyema wakajiongeza kama walivyofanya wengine ambao wanawalipa walimu wa kujitolea.
Aidha, hilo linaweza kwenda sambamba na kuchangia chakula, kwa ajili ya watoto wao, na kuachana na dhana kwamba, serikali ilishazuia michango yote shuleni na kusababisha watoto wao washinde njaa.
Wataalamu wa afya wanasema, kuwalisha chakula wanafunzi shuleni kunaongeza ulinzi wa kijamii, chakula na lishe kwa wanafunzi, kuimarisha mahudhurio shuleni na kukuza mchakato wa kujifunza.
Mkakati wa kulipa posho kwa walimu wa kujitolea, ujenzi wa shule, madarasa vikienda sambamba na kutambua umuhimu wa chakula, kwa ajili ya wanafunzi shuleni, itakuwa ni hatua nzuri ya kuboresha elimu.
Wakati serikali ikiendelea kuajiri walimu, ni vyema wazazi na walezi nao wakaendelea kukabili tatizo hilo kama wanavyofanya wengine kwenye baadhi ya wilaya na mikoa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED