Magufuli kukumbukwa Marekani, Ujerumani, Malawi

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 06:04 PM Mar 27 2025
Hayati John Magufuli kukumbukwa Marekani, Ujerumani, Malawi
Picha: Mtandao
Hayati John Magufuli kukumbukwa Marekani, Ujerumani, Malawi

Tamasha la Magufuli Festival linatarajiwa kuadhimishwa kwenye nchi nne, ikitajwa kuwa ni sehemu ya kumkumbuka na kumuenzi Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni miongoni mwa viongozi mashujaa wa Tanzania na Afrika.

Katika tamasha hilo pamoja na kumkumbuka Dk. Magufuli watu, pia wanatarajia kufanya maombi, viongozi wengine na taifa lote la Tanzania akiwemo Rais wa sasa  Samia Suluhu Hassan kwa mwendelezo wa sera za maendeleo.

Mwanzilishi wa taasisi ya kimataifa ya sanaa na utamaduni Kukaye Moto Culture mwanamuziki Arba Manillah anayeishi nchini Ujeruman, ambayo imeandaa tamasha hilo amesema kuwa wanamkumbuka Dk. Magufuli – Mwana wa Afrika aliyepigania maendeleo ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa ndani kwa wananchi wake.

Amesema Magufuli Fersitival linatarajiwa kuadhimishwa Machi 29 mwaka huu, katika nchi hizo ambapo taasisi hiyo ina ofisi zake, hivyo imejipanga kukutanisha baadhi ya watanzania na marafiki katika nchi ya Ujerumani, Malawi, Marekani na Tanzania.

Manillah ambaye amewahi kupewa Tuzo ya Amani Ujerumani alisema kuwa kuna kazi za Dk. Magufuli ambazo zinaishi na zinapaswa kuendelezwa ikiwamo jihidi zake za kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ngazi ya kimataifa.

Katika tamasha hilo kutawasilishwa mada kadhaa zenye kuelimisha na kuamsha uelewa kuendeleza utamaduni ikiwamo lugha ya kiswahili, historia, na urithi wa Afrika kama rasilimali za kuinua uchumi wa Tanzania na Afrika.

“Kupitia tamasha hili, tunatoa nafasi za mijadala yenye tija, ikichochea uzalendo na heshima kwa viongozi wetu wachapakazi wa Tanzania,” amesema Manillah

Mwenyekiti Kukaye Moto Culture Center nchini Tanzania Samson Karume amesema kwa hapa nchini litakuwa katika kituo hicho kilichopo Ubungo Makuburi, Dar es Salaam, linatarajiwa kutumika kuhamasisha vijana kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na badala yake kujituma kufanya kazi kwenye sekta tofauti ikiwamo ya Sanaa na utamaduni.  

“Kupitia kauli yake ya hapa kazi tu tunahamasisha vijana kuangalia fursa zilizopo kwenye sanaa na utamaduni kuzitumia katika kujipatia kipato na kuendesha maisha yao,” amesema Karume.   

“Pia tunatarajia baadhi yetu watakwenda kutembelea Kigamboni Women Sober House, kwenda kuzungumza wanaotibiwa athari za dawa za kulevya miongoni mwao wapo wasanii wanawake, tunaamini kuwatembelea na kuzungumza nao tunashiriki katika kuwapa tiba pamoja na kuwakumbusha kuwa jamii inawahitaji warejee jukwaani,” amesema Karume.