Stars: Uzoefu umeibeba Morocco

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:02 AM Mar 27 2025
Winga wa kimataifa wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Simon Msuva, akimtoka mchezaji wa Morocco (aliyelala chini), katika mechi ya Kundi E ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia iliyochezwa kwenye Mji wa Manispaa ya Oujda nchini humo
Picha; Mtandao
Winga wa kimataifa wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Simon Msuva, akimtoka mchezaji wa Morocco (aliyelala chini), katika mechi ya Kundi E ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia iliyochezwa kwenye Mji wa Manispaa ya Oujda nchini humo

BAADA ya timu yake kuchapwa mabao 2-0, Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Suleiman, amesema kipigo walichokipata dhidi ya Morocco kimetokana na 'uzoefu mkubwa' wa wapinzani wao na si vinginevyo.

Mabao ya Morocco katika mechi hiyo ya Kundi E ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia yaliyowekwa wavuni na Nayef Aguerd, dakika ya 51 na Brahim Diaz, aliyefunga kwa penalti dakika ya 58, na kufanya matokeo yajirudia kile kilichotokea katika mchezo wa mzunguko wa kwanza. 

Katika mechi hiyo ya kwanza iliyochezwa Novemba 21, mwaka juzi kwenye Uwanja Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Hakim Ziyech na Lusajo Mwaikenda, aliyejifunga ndio waliipata Morocco pointi tatu muhimu. 

Hata hivyo, kocha huyo maarufu kwa jina la Morocco, ambaye ni Mzanzibar amewasifu wachezaji wake na kusema walipambana 'kiume' katika mchezo huo. 

Kocha huyo alisema wapinzani wao walipata ushindi kwa sababu ya uzoefu, lakini kwa kiasi kikubwa walifanikiwa kuwadhibiti. 

"Niwashukuru wachezaji wangu, wamefanya kile ambacho tumekubaliana, kipindi chote cha kwanza tuliweza kuwadhibiti Morocco, tuliporudi kipindi cha pili hata sisi tulijua kitakuwa kipindi kigumu zaidi kuliko cha kwanza, tukajaribu kuhakikisha kile tulichokifanya tukifanye mara mbili zaidi, lakini nafikiri wameweza kutumia uzoefu wao zaidi kuhakikisha wanapata ushindi na wamefanikiwa," alisema Morocco. 

Aliongeza haikuwa rahisi kucheza na timu kubwa kama Morocco, huku matokeo yaliyopatikana ni matokeo halisi ya mpira wa miguu na hakuna mtu wa kumlaumu. 

"Mechi ilikuwa ngumu na kila mtu alijua na sisi mwenyewe tulijua hilo kuwa tunakuja kukutana na Morocco, moja kati ya timu ngumu sana Afrika na dunia kwa jumla, nafikiri tulikuwa na 'plan' nzuri tu, tulijitahidi kuhakikisha tunadhibiti presha yao kadri ya jinsi ilivyokuwa inawezekana. 

Narudia ilikuwa mechi ngumu lakini nawashukuru wachezaji wangu walicheza kwa maelekezo, mabao 2-0 ni matokeo halisi ya mpira wa miguu," alisema kocha huyo ambaye kwa mara ya kwanza alimwanzisha kipa kutoka JKT Tanzania, Yakuob Suleiman. 

Matokeo hayo yanaifanya Morocco kufikisha pointi 15, ikishinda michezo yote mitano ambayo imecheza, na kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakazochezwa mwakani katika nchi tatu tofauti ambazo ni Marekani, Mexico na Canada. 

Ikumbukwe kuwa Morocco ilifika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia katika fainali zilizopita ambazo zilichezwa nchini Qatar, ilitolewa na Ufaransa kwa kufungwa mabao 2-0. 

Taifa Stars bado ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita kama Niger, lakini ikiwa na idadi ndogo ya mabao ya kufunga. 

Kwa sasa matumaini pekee ya Taifa Stars kusonga mbele katika michuano hiyo yanabakia kuhakikisha inapata ushindi itakapowakaribisha nyumbani Niger na Zambia. 

Stars ilipata ushindi wa ugenini dhidi ya wenyeji Niger na baadaye ikapata pointi tatu muhimu kutoka kwa Zambia, lakini pia ilifungwa ilipokuwa ugenini Jamhuri ya Kideomrasi ya Congo (DR Congo).