Tamasha la Michezo ya Jadi kufanyika Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:58 PM Mar 24 2025
Mratibu wa Chama Cha Michezo ya Jadi Taifa Abubakary Kyaibamba akizungumza kwenye kikao na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya,mkoani Shinyanga.
Picha: Marco Maduhu
Mratibu wa Chama Cha Michezo ya Jadi Taifa Abubakary Kyaibamba akizungumza kwenye kikao na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya,mkoani Shinyanga.

Tamasha kubwa la Michezo ya Jadi linatarajiwa kufanyika mkoani Shinyanga Aprili 12, 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudumisha mila na tamaduni za Mtanzania.

Hayo yamebainishwa leo Machi 24, 2025, na Mratibu wa Chama cha Michezo ya Jadi Taifa (CHAMIJATA), Abubakary Kyaibamba, katika kikao na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya, mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kyaibamba, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhimiza masuala ya utamaduni, na amesisitiza kuwa katika maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 2025, wanautamaduni wanapaswa kushiriki katika sherehe hizo jijini Dodoma.

"Rais Samia ni muumini wa masuala ya utamaduni, ndiyo maana alicheza kwenye filamu ya Royal Tour na hata kushiriki katika shughuli za kimila akapewa jina la Chifu Hangaya. Amekuwa akisisitiza kufufuliwa na kuenziwa kwa michezo ya jadi," amesema Kyaibamba.

Kyaibamba ameeleza kuwa michezo ya jadi iliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1971 kwa lengo la kulinda utamaduni wa Mtanzania na kuhakikisha asili yake haipotei.

"Michezo ya jadi ni sehemu ya utambulisho wa Taifa. Taifa lisilo na utamaduni limepoteza asili yake. Michezo hii ni kielelezo cha Taifa na urithi wetu," amesema Kyaibamba.

Aidha, amesisitiza kuwa michezo hiyo ni fursa ya ajira kwa vijana, ikiwapa njia mbadala ya kujiingizia kipato na kuwaepusha na vitendo vya uhalifu, uvutaji wa bangi, na michezo ya kamari kama “betting”. Alitoa mfano wa mchezo wa Mbina (ngoma za jadi) kuwa sehemu ya utambulisho wa mkoa wa Shinyanga, wenye uwezo wa kuvutia watalii.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Shinyanga, Janety Elias, amesema kuwa michezo ya jadi ni nyenzo ya kuhifadhi mila na desturi za Mtanzania, pamoja na kurejesha maadili mema kwa jamii.

"Serikali ya Mkoa wa Shinyanga itaendelea kushirikiana na CHAMIJATA katika kufanikisha michezo hii na kuhakikisha tunadumisha utamaduni wetu," amesema Elias.Tamasha hilo litafanyika chini ya kauli mbiu:
 "Michezo ya Jadi ni kielelezo cha Taifa na Urithi wetu."