Arsenal Wanawake wapindua meza kibabe dhidi ya Real Madrid

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:47 PM Mar 27 2025
Arsenal Wanawake wapindua meza kibabe dhidi ya Real Madrid.
Picha: Mtandao
Arsenal Wanawake wapindua meza kibabe dhidi ya Real Madrid.

Timu ya wanawake ya Arsenal imeandika historia kwa kupindua matokeo dhidi ya Real Madrid kwa ushindi wa mabao 3-0, na kufanikiwa kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mchezo wa awali, Arsenal walikuwa wamepoteza kwa mabao 2-0, hali iliyowapunguza matumaini ya kufuzu. Hata hivyo, walionesha ujasiri wa hali ya juu katika mchezo wa marudiano uliopigwa Jumatano, wakiibuka na ushindi mnono wa 3-0 mbele ya mashabiki 22,517 katika Uwanja wa Emirates, na kufuzu kwa jumla ya mabao 3-2.

Alessia Russo alikuwa shujaa wa mchezo huo kwa Arsenal, akifunga mabao mawili, huku Mariona Caldentey akifunga bao la tatu kwa kichwa na kuihakikishia timu yake nafasi ya kucheza nusu fainali dhidi ya mabingwa mara nane wa Ligi ya Mabingwa, Lyon.

Arsenal wazima kujiamini kwa Madrid

Real Madrid walifika London wakiwa na ari kubwa baada ya kushinda El Clasico ya wanawake dhidi ya Barcelona kwa mara ya kwanza siku ya Jumapili. Hata hivyo, matumaini yao ya kufuzu nusu fainali yalizimwa na kiwango kikubwa cha Arsenal.

Kocha wa Arsenal alisema;

"Tulikuwa na imani kubwa wiki nzima. Tulijua tunachotaka kufanya, tulijua kile tunachoweza kufanya kama timu, na tumefanikisha hilo usiku wa leo."

Awali, Madrid walihatarisha kuongeza faida yao kwa jumla kabla ya mapumziko, lakini kipa wa Arsenal, Daphne van Domselaar, aliokoa shuti kali la Filippa Angeldahl na kudhibiti mashambulizi ya wapinzani.

Magoli matatu dakika 14 

Mabao matatu ndani ya dakika 14 za kwanza za kipindi cha pili yalibadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo.

Russo alifungua pazia la mabao sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza, akiunganisha krosi ya Chloe Kelly kwa ustadi mkubwa. Dakika tatu baadaye, Kelly alitoa pande safi kwa kiungo wa zamani wa Barcelona, Mariona Caldentey, ambaye alipachika bao la pili kwa kichwa.

Dakika za mwisho, Arsenal walihitimisha ushindi wao baada ya Real Madrid kushindwa kukabiliana na mpira wa adhabu uliopigwa ndani ya eneo la hatari, na Russo akafunga kwa sarakasi. Alikaribia kufunga hat-trick yake, lakini VAR ilifuta bao lake kwa kuotea.

Kwa ushindi huo wa kusisimua, Arsenal sasa wanajiandaa kupambana na Lyon katika hatua ya nusu fainali, wakisaka tiketi ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.