Dream Team FC, mshindi fainali Samia Cup

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 03:43 PM Apr 06 2025
Dream Team FC,  mshindi fainali Samia Cup
Picha: Julieth Mkireri
Dream Team FC, mshindi fainali Samia Cup

TIMU ya mpira wa miguu ya Dream team FC, imeibuka mshindi wa fainali za Samia Cup, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, baada ya kuifunga timu ya Wahenga FC magoli mawili.

Mechi ya fainali ya Samia Cup, ambayo ilifanyika katika viwanja vya Mji Mwema, ilihudhuriwa na mamia ya wananchi sambamba na wadhamini wa mashindano hayo kutoka Dar es Salam.

Mshindi wa fainali hizo ambaye ni Dream Team FC alinyakua kombe, Sh. milioni mbili pamoja na mbuzi watatu, huku mshindi wa pili Wahenga FC, akiondoka na Sh. milionI 1.5 na mbuzi.

Mshindi wa tatu ambaye ni Amazon FC, alikabidhiwa Sh. milioni moja na mbuzi wawili na mshindi wa nne Tandika FC, akiambulia Sh. laki tano na mbuzi mmoja.

Dream Team FC, mshindi fainali Samia Cup
Akikabidhi zawadi hizo Katibu wa Siasa, itikadi na Ujenzi Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga, amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo ambayo yanalengo la kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika michezo.

Bananga amewataka wadhamini kuendelea kudhamini michezo ambayo unachangia kuibua vipaji kwa vijana.

Dream Team FC, mshindi fainali Samia Cup
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kigamboni, Ramadhani Shauritanga, amewapongeza waandaaji na wadhamini wa mashindano hayo, huku akiwaomba kusaidia kuboresha viwanja vya mpira vinavyotumika katika mashindano mbalimbali .

Mmoja wa wadhamini wa mashindano hayo, Mohamed Haji, amesema wataendelea kudhamini mashindano ya michezo ambayo yanawakutanisha watu mbalimbali na kwamba, baada ya fainali hizo wanatarajia kuanza mashindano ya mpira wa mikono.