Katunda FC bingwa Katambi U-17 CUP

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:36 PM Apr 06 2025
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, akikabidhi kombe kwa Timu ya Katunda FC ambao wameibuka mabingwa mashindano ya Katambi U-17 CUP
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, akikabidhi kombe kwa Timu ya Katunda FC ambao wameibuka mabingwa mashindano ya Katambi U-17 CUP

MSHINDANO ya Katambi U-17 CUP, yametamatika rasmi, huku Timu ya Katunda FC wakiibuka washindi wa michuano hiyo, baada ya kuifunga Busulwa Sec, kwa mikwaju ya penati na kisha kuondoka na Kombe pamoja na kitita cha Sh. milioni moja.

Fainali hiyo imechezwa Aprili 4, 2025 katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Shinyanga SHYCOM, huku Mgeni Rasmi akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.

Mchezo huo umechezwa kwa kipindi cha dakika 90 na kuisha bila ya kufungana magoli na kisha kuchezwa mikwaju wa penati na hatimaye Katunda FC kuibuka na ushindi wa penati 4 kwa 3 dhidi ya Busulwa Sekondari.Aidha, mshindi wa tatu katika michuano hiyo akiibuka kuwa Ngokolo Sekondari.

Mtatiro akitoa zawadi kwa washindi, amemtangaza mshindi wa tatu ni Ngokolo Sekondari na wamepata Sh. 500,000; Mshindi wa Pili Busulwa Sekondari Sh. 700,000 na mshindi wa kwanza Katunda FC Sh,1,000,000.

Aidha, amempongeza Katambi kwa kuendelea kuiunga mkono michezo, na kwamba kupitia mashindano hayo amekuwa akiibua vipaji vya vijana.

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Hamisa Chacha, amesema michezo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi wa CCM, na kwamba Mbunge Katambi amekuwa wa mfano kuendelea kuitekeleza ilani hiyo, sababu michezo ni sehemu ya kuimarisha afya, kuibua vipaji pamoja na ajira.

Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA), Sylevester Budete, amempongeza Katambi, kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo pamoja na kudhamini, huku akimuomba aendelee na jitihada hizo za kuinua michezo Shinyanga.

Nao baadhi ya vijana ambao wameshiriki mashindano hayo, wamemshukuru Katambi kwa kuonesha vipaji vyao.

Mashindano hayo ya Katambi U-17 CUP, yalizinduliwa Februari 18, 2025 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, John Siagi, katika Uwanja wa CCM Kambarage na kushirikisha timu 16.