KLABU ya KMC, imefunga dirisha dogo la usajili kwa kuwaongeza wachezaji watano ambao imesema watakiongezea nguvu kikosi kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Khalid Chukuchuku, amesema jana kuwa wachezaji hao wamesajiliwa baada ya benchi la ufundi na viongozi kuona kuna umuhimu wa kufanya hivyo hasa baada ya matokeo ya mzunguko wa kwanza.
Chukuchuku, amewataja wachezaji wawili tu kati ya hao, ambao ni Hamad Pipino, akisajiliwa kutoka timu ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes na Deusdedith Okoyo akitokea Polisi Tanzania.
Mbali na kuichezea Polisi Tanzania, mchezaji huyo pia amewahi kuzichezea klabu za Geita Gold na JKT Tanzania.
Ingawa hakutaja wengine, lakini mmoja wapo ni straika wa zamani wa Simba na Azam, Shaaban Chilunda.
"Benchi la ufundi na viongozi waliona kuna umuhimu wa kukiongezea nguvu kikosi, hasa kutokana na matokeo tuliyoyapata kwenye mzunguko wa kwanza hivyo tukalazimika kwenda sokoni kutafuta baadhi ya wachezaji kwa ajili ya kutuongezea nguvu, leo nitawataja wawili ambao ni Pipino aliyetokea timu ya Ngorongoro Heroes ambapo amekuwa na mchango mkubwa, tukaona bora tumsajili, mwingine ni Okoyo akitokea Polisi Tanzania," alisema Ofisa Habari huyo.
Mbali na hao, alisema wachezaji wengine watawaweka kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii wakati wowote kuanzia sasa.
"Ukiacha hao, kuna straika mkubwa tu ambaye tutamtangaza wakati wowote kuanzia sasa, tunakamilisha vitu vichache, ameshawahi kuichezea Azam FC, Simba na amecheza ligi nje ya nchi," alisema Chukuchuku, akimaanisha Chilunda.
"Tumewasajili wachezaji wa Kitanzania waliokuwa wanacheza Ligi Kuu nchini Malawi kwa ujumla tumefanya usajili wa wachezaji watano, mashabiki wengi hawawafahamu lakini ni wachezaji wazuri watu watawaona muda utakapofika," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED