WAKATI Simba ikiandaa kaulimbiu mpya kuelekea katika michezo yake miwili ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, iliyopewa jina la 'Hii Tunavuka', ili kutoa hamasa kwa wanachama na mashabiki, watani zao, Yanga imetamba wanaandaa 'dozi' watakapoikabili Songea United hapo kesho, imeelezwa.
Mbali na viongozi na wachezaji wakitaka kuvuka hatua ya robo fainali kwa kuikabili Al Masry ya Misri, pia leo wanataka kuona wanasonga mbele kwenye michuano ya Kombe la FA watakapowakaribisha Bigman FC inayoshiriki Ligi ya Championship.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema, 'Hii Tunavuka' ni kauli mbiu kwa ajili ya michezo mwili ya nyumbani na ugenini dhidi ya Al Masry, huku akibainisha wanakwenda kucheza mechi ngumu.
"Tumejiandaa iwe jua, iwe mvua, safari hii tunataka kuvuka kutoka robo fainali ambao tumekuwa na mkwamo nayo kwa takribani miaka mitano, safari hii tunataka kwenda nusu fainali. Robo fainali zote tulikuwa tunazichukuliwa kama mafunzo kwetu, sasa tumeshajifunza, kwa maana hiyo pamoja na kwamba tuna kauli mbiu yetu inayofanya vizuri sana ya 'ubaya ubwela' lakini hii ni kwa ajili ya mchezo huu tu," alisema Ahmed.
Alisema kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka nchini kesho alfajiri kuelekea Cairo na baadaye Ismailia watakapoikabili Al Masry ifikapo Aprili 2, mwaka huu.
Aliongeza wachezaji sita wa kikosi hicho waliokuwa katika na kikosi cha Taifa Stars hawatarejea nchini, badala yake wataondoka Morocco moja kwa moja na kwenda Misri kuwasubiri wenzao, na kuweka wazi wataukosa mchezo wa leo dhidi ya Bigman.
"Wachezaji waliokuwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ni Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', Shomari Kapombe, Abdulrazack Hamza, Kibu Denis na Yusuph Kagoma, wao watasafiri moja kwa moja kwenda Misri, wao tutawakuta huko huko. Wengine ni Steven Mukwala aliyekuwa kwenye kikosi cha Uganda na Moussa Camara aliyekuwa kwenye kikosi cha Guinea, baada ya mechi yao iliyochezwa Kampala, Uganda ikishinda bao 1-0, wameshawasili nchini na wapo kambini.
Tumekuwa na wiki mbili thabiti za maandalizi kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Bigman, pamoja na kwamba ni timu ngeni kwenye masikio yetu, lakini haiondoi ukweli ni mechi ngumu," alisema meneja huyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, amesema anatarajia kupata ushindi mnono katika mchezo dhidi ya Songea United utakaochezwa keshokutwa kama wachezaji wake ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara wataonyesha kiwango alichokiona katika mechi ya kirafiki dhidi ya Singida Black Stars.
Miloud alisema licha ya timu yake haikuwa na wachezaji zaidi ya 10 tegemeo, huku Singida Black Stars ikichezesha kikosi chake kamili, lakini walikabiliana nao vyema na hakuna pengo lililoonekana.
"Tulikwenda Singida bila wachezaji 10 tegemeo, hivyo kwetu ilikuwa ngumu sana, lakini walicheza vyema dhidi ya timu yenye wachezaji bora iliyokamilika ya Singida Black Stars, kwa maana hiyo hawa wachezaji kama nikiwachezesha dhidi ya Songea United wanaweza kunipa ninachokihitaji.
Tunakabiliwa na uchovu, nadhani hata wachezaji watakaotoka kwenye vikosi vya timu za taifa pia watakabiliwa na uchovu, kwa maana hiyo katika mchezo huo nitatengeneza mazingira ya 'kubalansi' kuchezesha nyota ambao wamepumzika na dakika chache wale ambao wametoka kwenye mechi za kimataifa na kusafiri kwa umbali mrefu," alisema kocha huyo.
Aliongeza kwa sasa ameshakiandaa kikosi chake kwa ajili ya kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya FA.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo ikibeba taji hiloo Juni 2, mwaka jana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, baada ya kuifunga Azam FC penalti 6-5 kufuatia matokei ya suluhu waliyopata ndani ya dakika 120.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED