NI kama vile timu ya Simba imerahisishiwa katika harakati zake za kufanya vyema kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) dhidi ya Al Masry, kutokana mchezo huo kuchezwa kwenye mji wa Suez, badala ya Ismailia ambako ndipo nyumbani kwa wapinzani wao.
Akizungumza kutoka mjini Ismailia, mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally, amesema kuwa aliwauliza Wamisri ni kwa nini mechi yao dhidi ya Al Masry imepelekwa kwenye mji huo wa Suez ambao uko mbali na wenyeji wao, walimwambia ni kutokana na ukorofi wa mashabiki wa timu hiyo.
"Nilipofika hapa niliuliza kwa nini hawa Al Masry wameupeleka mchezo wetu mji za Suez, wakaniambia mamlaka za soka zimeamua hivyo kutokana na ukorofi wa mashabiki wao, ni wakorofi sana na wameshawahi kufanya fujo kwenye michezo kadhaa, ndio maana hiyo mechi imehamishiwa huko," alisema Abbas.
Hata hivyo alisema umbali wa kutoka Ismailia hadi Suez si zaidi ya kilometa 80 na ni mwendo wa masaa mawili barabarani.
"Najua baadhi ya mashabiki watakuja, lakini itapunguza ule utukutu wao kwani watajiona kama wako ugenini na sisi tuko ugenini pia," alisema Abbas.
Aidha, alisema sababu nyingine ambayo anaona wamerahisishiwa kazi na mazingira mazuri kuelekea mchezo huo ni kupewa uwanja bora wa kufanyia mazoezi ambao hakuna timu yoyote inaruhusiwa kucheza zaidi ya mechi tu.
Alisema uwanja huo unaitwa Suez Canal Authority, ambao ni moja kati ya viwanja vyenye ubora wa hali ya juu si nchini Misri, bali Afrika nzima.
"Huu uwanja hata wenyewe hawautumii kwenye mechi za kawaida, ni zile mechi kubwa tu, majuzi ulichezewa mechi ya kufuzu CHAN, kati ya Misri na Afrika Kusini ulichezewa kwenye uwanja huu, lakini sisi Simba tumeruhusiwa tufanye mazoezi kwa siku tatu.
Kuna viwanja vingine nje vizuri tu vya kufanyia mazoezi ambavyo timu zingine huwa zinafanyia, lakini sisi Simba tumeambiwa tufanyie kwenye uwanja huu mkubwa," alisema.
Alisema sababu kubwa ni ukubwa na umaarufu wa timu ya Simba nchini humo.
"Wala sikupata shida, nilipokuja kuuomba huu uwnaja na kuwaambia ni timu ya Simba, moja kwa moja wakaruhusu, na wakaniambia kama ingekuwa timu zingine tusingewaruhusu, uwanja mkubwa huwa haufanyiwi mazoezi, bali mechi tu na ni mechi chache mno," alisema mratibu huyo.
Kuhusu kuondoka mjini Ismailia kwenda mji mdogo wa Suez, alisema kikosi kitaondoka kesho Jumanne kwa matakwa ya Kocha Mkuu, Fedlu Davids, ambaye alitaka kikosi chake kifanye mazoezi kwenye uwanja ambao mechi itachezwa, siku moja kabla.
"Tungekuwa na uwezo wa kutoka hapa moja kwa moja kwenda kwenye mechi siku hiyo hiyo, lakini kocha akasema tuondoke siku moja kabla ili wachezaji wake wakafanye mazoezi, wakauone na uwanja ambao watautumia," alisema.
Simba itaingia dimbani, kesho kutwa saa 1:00 usiku kucheza mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya timu hiyo na mechi ya marudiano inatarajiwa kupigwa, Aprili 9, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED