Yanga kuivaa Tabora United bila nyota wake wanne

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:35 PM Apr 02 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, amethibitisha kuwa katika mchezo wa leo dhidi ya Tabora United, atawakosa wachezaji wanne kwa sababu mbalimbali, ikiwemo uchovu baada ya kutoka kutumikia vikosi vyao vya timu za taifa pamoja na majeraha.

Akizungumza wakati wa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaotarajiwa kupigwa leo, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, amewataja wachezaji watakaokosekana kuwa ni Stephane Aziz Ki, Clatous Chama, Kennedy Musonda na Khalid Aucho.

Aziz Ki, amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo wakati watatu waliobaki wakiwa na uchovu kutokana na kutumika kwenye vikosi vyao vya timu za taifa zilizokuwa zikisaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani katika nchi za Marekani, Mexico na Canada.

Kocha huyo amesema maandalizi ya mchezo yameshakamilika, kilichobaki ni kwenda kuwaonyesha watu ukubwa wa Yanga.

"Tumejiandaa, nadhani katika mchezo huu tutaonyesha ukubwa wetu. Tumejiandaa kwa mchezo huu kama vile tunakwenda kucheza moja kati ya mechi kubwa za Ligi Kuu au za kimataifa kwa sababu tunahitaji pointi tatu, pia tunajua tunakwenda kucheza mechi ngumu," alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa anafahamu ugumu wa mchezo huo, kwani Tabora United ni moja kati ya timu chache zilizoifunga Yanga.

"Sisi kama Yanga kila timu inayocheza na sisi inakuja kwa nguvu ili kutuzuia, lakini Tabora United ni moja kati ya timu ngumu kwenye Ligi Kuu, nina uhakika kwa jinsi nilivyowafundisha wachezaji wangu na tulivyoongea naamini watatupa ushindi," alisema.

Yanga itaingia uwanjani na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 3-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa uwanja wa Azam Complex, Novemba 7 mwaka jana.

Kwa upande wake, Kocha wa Tabora United, Genesis Mang'ombe, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo

"Tupo tayari kwa mchezo huu, hatuna majeruhi, tunakwenda kuwapa mashabiki mechi nzuri, tumefanya kila kitu kuhakikisha tunashinda mchezo huu," alisema kocha huyo mpya ambaye amechukua mikoba ya Anicet Makiadi.

Yanga inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa kileleni kwenye msimamao wa ligi ikiwa na pointi 58, huku Tabora United, ikisaka nafasi ya nne ili kucheza mechi za kimataifa msimu ujao ambapo kwa sasa inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 37.