KIWANDA cha Ubungo Farm Implements (UFI) cha Ubungo, Dar es Salaam kilichokuwa kinazalisha zana za kilimo kimebinafishwa, hivi sasa hakizalishi tena zana hizo, kinazalisha mabomba ya maji.
Ni hali inayokinzana na dhamira ya mwasisi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye serikali yake ilikianzisha mwishoni mwa miaka ya 1960 kwa lengo la kuzalisha zana za kilimo ili wakulima wawe na uhakika wa kuzipata kwa urahisi nchini na kwa bei nafuu.
Kukiwa na mabadiliko hayo ya matumizi ya kiwanda, kwa miaka 26 baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda cha UFI ambacho hivi sasa kinaitwa TSP, wanasotea haki zao.
Wanadai wameshaandika zaidi ya barua 40 kwa mamlaka mbalimbali nchini tangu mwaka 1998 bila mafanikio yoyote. Hadi kiwanda kinabinafisishwa mwaka 1998, kilikuwa na wafanyakazi 508 wanaodai stahiki zao za malipo ya mishahara, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na posho nyinginezo.
Taasisi ambazo wamekuwa wakielekeza barua zao kushughulikia madai yao ni pamoja na Bunge na Ikulu. Hata hivyo, wanadai hawajui tarehe ya kulipwa stahiki zao.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Ufuatiliaji Mafao ya Wafanyakazi wa Kiwanda cha UFI, Makamba Kigome, wanachodai ni kupunjwa katika malipo ya mtumishi na familia zao - kwamba hayakulipwa kulingana na umbali wa kila mmoja anakotoka, pia kutozingatiwa ngazi ya mshahara wa mtumishi.
Madai mengine ni posho ya kufungasha mizigo; haikuwafikia watumishi licha ya kuwapo kwenye mchanganuo wa malipo ya UFI.
Hoja zingine ni kutofuatwa Mkataba wa Hali Bora Sehemu ya Kazi, malimbikizo kulipwa kwa kutofuata mabadiliko ya mishahara tangu Julai 1994 hadi Julai 1998, kutolipwa malimbikizo ya likizo badala yake walilipwa likizo moja pekee ya mwaka 1994.
Wafanyakazi hao pia wanadai posho ya kujikimu kwa kipindi cha miezi mitatu wakati wanasubiri kulipwa mafao ya kuachishwa kazi. Barua zao zimeelekezwa kiwanda cha UFI wakati huo, Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) na uliokuwa uongozi wa UFI.
Tunafahamu kuhusu barua yao ya Februari 14 mwaka huu waliyomwandikia Spika wa Bunge, Dk. Tulia Askon. Maudhui yake yanahusu wafanyakazi 271 wa kiwanda cha UFI, wanaoeleza kuwa baada ya mchakato wa ubinafsishaji, walilipwa sehemu ya malimbikizo ya mishahara ya miezi sita.
Wanadai hakuwalipwa mafao ya wafanyakazi licha ya kuwa wametimiza masharti ya kuwa kulipwa mafao, yaani walikuwa wametumikia kiwanda zaidi ya miezi 120 (kwa vigezo vya Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na NPF wakati huo.
Kimsingi, wafanyakazi wanada haki zao za msingi kwa kuwa walijiunga katika mifuko ya jamii ya PPF na NPF na wakachangia michango yao kutoka katika mishahara yao kwa mujibu wa sheria.
Ni vyema mamlaka husika zikamaliza suala hilo sasa kwa kuwa walishafikisha malalamiko yao sehemu mbalimbali, zikiwamo Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Waziri Mkuu. Baadhi wamefariki dunia pasi na kulipwa stahiki zao.
Ofisi ya Spika ambayo wameshaiandikia, isadi kundi hili kupata stahiki zake kwa kuwa madai hayo ni ya muda mrefu ilhali wahusika wanalalama kuishi katika hali ngumu inayohatarisha maisha yao na familia zao.
Hoja za wafanyakazi hawa wa zamani wa kiwanda cha UFI zifanyiwe kazi na mamlaka husika za serikali ili kutenda haki kwa kundi hili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED