Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amependekeza Ushoroba wa Lobita kutoka Angola hadi Dar es Salaam upewe jina la Lobito – Dar, ili kusadifu uwezo wa reli ya kuunganisha Bahari za Atlantiki na Hindi.
Ushoroba huo unaunganisha nchi na nchi kuanzia Bahari ya Atlantiki kwa upande wa Angola hadi Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Machi 27, 2025 katika Mkutano wa Mpango wa Mattei wa Afrika, Italia kuhusu Reli kuziunganisha Bahari za Atlantiki na Hindi, amesema mpango wa ushirikiano wa Maendeleo wa Italia na Afrika (Matttei Plan for Africa) unatarajiwa kuboresha miundombinu ya maendeleo Afrika kwa kuunganisha reli ya ushoroba huo.
Ushoroba wa Lobito umeunganishwa na miundombinu ya reli kwa nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Zambia.
Akizungumza katika mada kuu ya mkutano huo ya uwekezaji katika miundombinu barani Afrika kupitia Ushoroba wa Lobito, Waziri Kombo ameipongeza Italia kwa mpango huu utaoibua fursa za kimkakati katika sekta za, biashara, uwekezaji, kilimo, madini pamoja na teknolojia kwa kuiunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Ushoroba wa Lobito.
“Tanzania ni tajiri wa ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kuwanufaisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Kiitaliano katika kilimo haswa kilimo cha kahawa. Uwekezaji utakaosaidia kupunguza changamoto zinazolikumba bara la Ulaya, ikiwemo uhamiaji haramu unaochochewa na ukosefu wa ajira kwa vijana wa Afrika,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED