Maafisa Mawasiliano wa Serikali wakumbushwa kuendelea kuzingatia alama za taifa ambazo zipo kwa mujibu wa sheria ili mabadiliko ya teknolojia yasiathiri uwepo wa alama hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali George Lugome wakati akitoa wasilisho katika Mkutano wa Mkuu wa 13 wa Mwaka wa Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) uliofanyika Mkoani Morogoro jana Aprili 08, 2025
Amefafanua kwamba katika kuhabarisha umma kuna wakati afisa anaamua kujiongeza na hivyo kuenenda kinyume na sheria ambazo zinalinda alama hizo za taifa ikiwemo bendera ya taifa, ngao ya taifa na wimbo wa taifa.
“Bendera yetu tunayotumia sasa ilianza kutumika Mwaka 1964 baada ya muungano na ina rangi nne, ambazo ni rangi ya kijani, bluu na hizo rangi zinatenganishwa na rangi nyeusi ambayo itakuwa imetenganishwa na ufito wa rangi ya dhahabu” alieleza
Ukisoma sheria ya Ngao na Bendera ya Taifa ya Mwaka 1971 imeweka makatazo mbalimbali, ili kulinda nembo hizo za taifa, sisi watu wa mawasiliano tunapokuwa tunafanya kazi zetu za kutangaza lazima tutumie alama hizo kwa usahihi.
Aidha, ameongeza kuwa, kuna mchanganyiko wa rangi kwenye kila rangi ya bendera ili kupata rangi halisi za bendera ikiwa pamoja na kuzingatia uwiano sahihi katika kupata urefu na upana wa bendera ya taifa.
Ameeleza kwamba, Kamba za kufunga bendera ambazo zinapaswa kuwa njano, bluu au kijani lakini kwa Kamba nyeupe au nyekundu itatumika kwa bendera ya Rais au Jeshi la Wananchi.
Akizungumzia kuhusu wimbo wa taifa Bw. Lugome ameeleza kwamba, wimbo wa taifa ukiwa unaimbwa watu hawatakiwi kuweka mkono kifuani kuonesha utaifa ila inashauriwa kushusha mikono chini na kuzingatia kuimba kwa ala zilizowekwa bila kuongeza chochote.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa umma tukiamini kwamba na nyinyi maafisa mawasiliano wa serikali mtaenda kutoa elimu katika maeneo yenu ili kuhakikisha tunazingatia matumizi sahihi ya alama za taifa” alisisitiza
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanataaluma wa Uhusiano na Umma Tanzania (PRST) Assah Mwambene amesema nembo ya taasisi ndio inayoonesha maono na dhamira ya taasisi unayoifanyia kazi.
“Ni vyema kukaandaliwa muongozo wa matumizi ya nembo za taifa na kuainisha maeneo maalumu ambayo kama taasisi inauhitaji kupata alama hizo za taifa ipate alama sahihi”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED