Oliver Kisaka aibuka mshindi uchaguzi wa CHADEMA Korogwe Vijijini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:43 PM Apr 17 2025
news
Mtandao
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Korogwe Vijijini, Oliver Kisaka.

MWANACHAMA wa CHADEMA,Oliver Kisaka maarufu Solo Mnamunga ameibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa marudio wa Mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Korogwe Vijijini.

Uchaguzi wa marudio kwa ngazi zote za chama hicho kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini, umefanyika Jumatatu Aprili 14,2025 baada ya ule wa Novemba 8,2024 kufutwa na CHADEMA Kanda ya Kaskazini pasipo kuweka wazi sababu. 

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Tanga, Wakili Rachael Kiogwe amemtangaza Kisaka kuwa mshindi wa kira 67,akifuatiwa na Rajabu Magogo aliyepata kura 20 huku Aurelian Nziku akiambulia kura tisa.

Kiongwe ambaye pia ni Katibu wa BAWACHA Kanda ya Kaskazini, amemtangaza Thomas Lwoga kuwa Katibu wa Jimbo baada ya kushinda kwa kura 82 akifuatiwa na Salim Sempoli kura 14.

Nafasi ya Katibu Mwenezi imeenda kwa Ibrahim Wassi aliyepata kura 83, huku Luciana Hizza akiambulia kura 11,na Mjumbe wa Mkutano Mkuu mshindi ni Peter Lameck aliyepata kura 67.

Kwa nafasi ya Mweka Hazina mshindi ni Twaha Kidiwa aliyepata 90,huku BAWACHA  Emmy Kangaulaya ameibuka mshindi kwa kura 20.

Licha ya uchaguzi kuchelewa kuanza,wajumbe toka kata 17 walioshiriki uchaguzi walisubiria matokeo mpaka saa 2 usiku.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi huo,Mwenyekiti Kisaka amesema: "Kwanza namshukuru Mungu maana haikuwa rahisi,pili nawashukuru viongozi waliomaliza mda wao kwani bila wao basi CHADEMA Korogwe isingekuwa na mwamko namna hii, naahidi kuleta mageuzi makubwa kwenye jimbo letu ikiwemo kuhakikisha chama kinakuwa na wawakilishi wa serikalini kama madiwani na wabunge,"amesema.

Kuhusu mwelekeo wa CHADEMA amesema: "Jambo muhimu kuliko yote ni kuhakikisha kila mmoja ana pambana ili kupata mabadiliko yatakayopelekea kuwa na chaguzi huru na haki."

Aidha,amesema kwa sasa Korogwe Vijijini wanaandaa ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche mapema mwisho wa mwezi huu huku akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono operesheni ya 'No Reforms No Election’ na kuchangia chama kupitia TONE TONE.