DC: UKIMWI bado upo, chukueni tahadhari

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 10:09 AM Dec 03 2024
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga.

WANANCHI mkoani Mbeya wametakiwa kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa UKIMWI kwani bado upo licha ya juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga, alitoa wito huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika juzi wilayani humo.

Batenga alisema msingi wa kwanza wa mtu ni kuwa na afya njema kwani maendeleo pesa na mambo mengine yanapatikana kwa kuwa na afya njema na kwamba licha ya kuwapo dawa za kufubaza makali ya VVU lakini bado tiba na chanjo ya ugonjwa huo bado haijapatikana.

“Tiba ya UKIMWI bado haijapatikana wala chanjo, tukilitambua hilo tutaendelea kujikumbusha kwamba UKIMWI bado upo, hivyo tuishi kwa kujikinga na kuchukua tahadhari, tuepuke tabia hatarishi zinazoweza kusababisha kupata maambukizi,” alisema Batenga.

Aliwataka wananchi kuendelea kujitokeza kupima afya zao ili watakaogundulika kuwa na maambukizi waanze kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU pamoja na kupata mbinu za kuepuka maambukizi mapya.

Pia, alitoa wito kwa wanaume kujitokeza kupima afya zao badala ya kutegemea vipimo vya wake zao, kwamba  majibu ya wake zao ndiyo majibu yao kwani jambo hilo siyo sahihi  na kwamba afya ni jambo la mtu binafsi na siyo jambo la familia.

“Wanaume acheni kutembea na majibu ya vipimo vya wake zenu hasa yanapokuja majibu mazuri, hiyo kwani anayepata ugonjwa huu ni mtu na siyo familia, mke anaweza kuwa mzima na wewe ukawa na maambukizi, hivyo kila mtu akapime yeye mwenyewe ajue afya yake,” alisisitiza.

Awali akitoa salamu katika maadhimisho hayo, Diwani wa Kata ya Ifumbo, Weston Mpyila alishukuru maadhimisho hayo kufanyika katika Wilaya ya Chunya kimkoa, akisema imekuwa nafasi nzuri ya wao kujifunza  kupitia mada mbalimbali kutoka kwa wadau na wataalamu.

Akisoma taarifa ya hali ya utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI Mratibu wa Huduma za UKIMWI Mkoa wa Mbeya, Dk. Deo Magongwe, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa katika jamii na kuijulisha jamii kufahamu mafanikio na vikwazo vinavyoikabili dunia.