Kaka wa Mwenyekiti CCM Mkoa achinjwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:36 AM Dec 03 2024
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP) Simon Maigwa.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP) Simon Maigwa.

ISAACK Mallya, ambaye ni kaka wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, ameuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga kichwani na shingoni baada ya kuvamiwa nyumbani na watu wasiojulikana.

Mallya, mkazi wa kijiji cha Umbwe Onana, Kobosho, wilayani Moshi, aliuawa jana saa mbili asubuhi.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP) Simon Maigwa alithibitisha kuuawa kwa mtu huyo, huku akieleza kwamba chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana.

"Ni kweli tukio hilo limetokea Desemba 2 mwaka huu katika Kijiji cha Umbwe Onana. Jeshi la Polisi linafuatilia kuona chanzo cha tukio hilo.

"Tunawaomba wananchi waache kuchukua sheria mkononi ili kupunguza mauaji yasiyo na hatia. Lakini niseme tu kwa sasa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini (KCMC)," alisema.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa CCM, Kilimanjaro, Boisafi, alikiri marehemu Isaack Mallya, ni ndugu yake, kwa maana ya mtoto wa baba mkubwa.

"Ni ndugu yangu, ni mtoto wa baba yangu mkubwa, tumeishi wote, mji mmoja na mahali alipouawa, ndipo nimekulia hapo. Ni jambo la kikatili sana limefanyika katika jamii.

"Hata kama mtu ni mkorofi au nini, kitu kilichofanyika kinakemewa na kila mtu, yaani jambo lililofanyika ni la aibu, mtu kuamua kuchukua uamuzi wake kwenda kumuua mtu, tena nyumbani kwake.

"Kama walikuwa wanamdai, wangesema tungelipa, lakini kitu walichokifanya, kusema ukweli ni ukatili. Tunakemea jambo hili na lisijirudie kwa watu wengine, ni jambo linalosikitisha sana, kwani linajenga hofu hasa kipindi hiki ambacho tunaelekea sikukuu za mwisho wa mwaka," alisema. 

Boisafi aliongeza, "Matukio haya yanayotokea, yanatisha hata wale ndugu zetu na marafiki zetu ambao watasafiri kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi kuja Kilimanjaro.

"Mambo haya yanatia doa Mkoa wa Kilimanjaro na jamii yote inayotuzunguka. Lakini ninaamini Jeshi la Polisi litafanya bidii kuchunguza matatizo yaliyotokea na kuwatafuta waliohusika na jambo hili ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake." 

WALIANZIA MIFUGO 

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro alisema mauaji hayo ya kaka yake yamemsikitisha, akikumbusha kuwa, "Kipindi cha nyuma kuna mifugo iliuawa, walikwenda kukatakata ng'ombe wake, inawezekana wakati huo ndio walikuwa wakimtafutia 'timing' (kumvizia), ikawa tofauti. 

"Maana muda ambao nimepata habari ni kipindi cha asubuhi, ambapo kwa kawaida huwa anahangaika na mifugo yake, halafu baadaye anakwenda kanisani," alidai. 

Ndugu mwingine wa marehemu Isaack, ambaye ni mfanyabiashara maarufu katika Mji wa Moshi, Baraka Mallya, maarufu Fresh Coach, alisema: "Huyo aliyeuawa ni ndugu yangu, yaani ni tukio la kinyama kabisa kuwahi kutokea pale kijijini.

"Boisafi na huyo Isaack (marehemu), ni mtu na kaka yake. Ni mtu wa karibu sana na familia hiyo, Boisafi amekulia kwenye familia ya baba yake na marehemu Isaack.

"Huyo Isaack alitaka Boisafi, akasome seminari ili baadaye aje awe padri, kwa sababu alikuwa ni kijana mwenye akili sana pale kijijini. Huyo marehemu Isaack zamani alikuwa mfanyabiashara lakini alirudi kijijini. Hapo alipouawa, ni nyumbani kwa baba yake Isaack kabisa," alisema mfanyabiashara Baraka.

Mmoja wa majirani, Manka Kipesa, ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi, alisema majira ya asubuhi alifika katika eneo hilo kwa ajili ya ununuzi wa ndizi mbichi, baada ya kutoka katika nyumba nyingine na ndipo aliposhuhudia ukatili huo.

"Nilifika nyumbani hapo kwa ajili ya kutaka ndizi baada ya kutoka nyumbani nyingine kununua, nimefika hapa nikamkuta akichuruzika damu, ndipo nilipopiga kelele na majirani wakaja ingawa alipoteza maisha muda huohuo kabla ya kukimbizwa hospitalini," alidai.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Vicky Massawe, alisema alifika eneo la tukio hilo baada ya kupata taarifa na alipofika alikuta tayari Isaack ameshafariki dunia.

"Tupo kwenye siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia lakini tunaona matukio ya ukatili yakiongezeka. Hivyo, niombe serikali kupitia wataalamu wake kutoa elimu zaidi na kusaidia jamii, hasa wenye msongo wa mawazo, ili kupunguza matukio hayo.