ABDUL Nondo amepatikana akidaiwa kutupwa ufukweni. Chama cha ACT Wazalendo kimehoji maswali matano kwa Jeshi la Polisi kufuatia madai ya kutekwa kwa Mwenyekiti wake huyo Ngome ya Vijana Taifa.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, akiwa katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam jana alikomtembelea kumjulia hali, alidai Nondo amepigwa na kuumizwa. Kwa hali aliyokuwa nayo, hakuwa na uwezo wa kuzungumza vizuri.
Alisema Nondo alimsimulia kwa shida kilichojiri baada ya kutekwa juzi alfajiri kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli; kwamba alifungwa kitambaa cheusi na kupigwa sana huku akitishiwa kuuliwa.
"Maelezo yake ni kwamba, alipotolewa pale Stendi ya Magufuli, alifungwa kitambaa, hivyo hakuwa anaona. Baada ya hapo amekuwa akipigwa muda mrefu, baadaye walisitisha kwenye eneo ambalo halifahamu kisha alitupwa pale Coco Beach ambako walimfungua kitambaa na pingu na baadaye akabaini yuko eneo hilo na akaomba msaada," alisimulia Mchinjita, kama alivyodai kuelezwa na Nondo.
Alipoulizwa kuhusu alichokuwa akiambiwa na wanaotajwa "watekaji", Mchinjita alisema, "Maelezo anayatoa ni kwamba alipigwa na alikuwa kwenye kitisho cha kifo na yeye alipopelekwa pale Coco Beach na pale baharini alijua ni hatima yake kwa sababu alikuwa amefungwa na wakamwacha kwenye eneo hilo, lakini baadaye akatishwa tu kwamba akikamatwa tena, basi hawatomwachia."
Mchinjita alidai Nondo alikutwa eneo hilo saa nne na nusu usiku wa kuamkia jana ndipo wasamaria wema walimchukua na kumpeleka makao makuu ya chama hicho Magomeni, wilayani Kinondoni kisha kukimbizwa hospitalini.
Alisema kuwa alipomtazama, aliona ameumizwa maeneo ya miguuni, kifuani, mgongoni na mikono yake ilikuwa inaonesha ilifungwa kwa muda mrefu. Imevimba.
"Madaktari wamesema taarifa ya uchunguzi ya awali hajavunjika, wanaendelea na matibabu lakini wametuambia watatoa taarifa kesho (leo) baada ya madaktari bingwa kuja, lakini kwa sasa wamekwenda kumlaza katika chumba cha upasuaji," alidai Mchinjita.
Alisisitiza kupatikana kwa taarifa za kutekwa kwake mapema na hata kugundua gari lililotumika kufanikisha utekaji, kumesaidia kupatikana haraka kwa kuwa wapo vijana wengi waliotekwa nchini na hawajapatikana.
Kiongozi wa Chama mstaafu, Zitto Kabwe alisema wakiwa mkoani Kigoma na Nondo wakati wa kampeni za uchaguzi uliokamilika Novemba 27, mwaka huu, hakuwahi kutishwa kwa namna yoyote ile.
Aliongeza kuwa hakufanya jambo lolote baya ambalo pengine linaweza kuwa sababu ya kutekwa kwake huku akisisitiza atakapopata nafuu atasimulia ili kupata funzo la namna ya kukabiliana na matukio hayo.
Nondo anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana juzi alfajiri akiwa kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli iliyoko Mbezi Louis, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
MASWALI MATANO
Naibu Katibu wa Ngome ya Vijana vya chama hicho, Ruqayya Nassir amelitaka Jeshi la Polisi kujibu maswali matano, ikiwamo kueleza zile pingu zilizoanguka na kuokotwa na mashuhuda katika tukio hilo ni za nani kwa kuwa haziuzwi kama karanga wala njugu?
Pili; amelitaka jeshi hilo litaje hatua lilizochukua kuhusiana na taarifa za awali kuhusu aliyemtaja kwa jina kuwa ndiye mmiliki wa gari lililotumika kumteka Nondo.
Hoja nyingine ya chama hicho ni kutaka kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya Kituo cha Polisi Gogoni ambako inadaiwa gari lililotumika katika utekaji ni la kituo hicho.
"Je, mpaka sasa jeshi limewabaini ni polisi waliomteka, kumpiga na kumtelekeza Nondo?" alihoji Ruqayya na kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura kutoa majibu aliyoyaita "yenye mashiko kutokana na suala hilo".
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED