Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea na kampeni yake ya nyumba kwa nyumba ya kutoa elimu kuhusu faida na matumizi ya umeme pamoja na kuhamasisha wananchi kuunganisha umeme.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo kwa Mkoa wa Tabora, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Jaina Msuya amesema kuwa kampeni hiyo ni muendelezo wa juhudi zinazofanywa na Wakala huo kuhakikisha kila mwananchi aliyepo ndani ya wigo wa mradi umeme vijijini anaunganisha umeme.
“Nia ya Serikali ni kuwaletea maendeleo wananchi wote pamoja na wa vijijini ndo maana imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali kwa gharama kubwa ukiwemo mradi huu wa kusambaza umeme vijijini.
Tumekuja na kampeni hii ya kutembelea nyumba kwa nyumba kila kijiji kuzungumza na wananchi waliofikiwa na mradi na bado hawajajiunga. Lengo ni kujua changamoto wanazopitia na kuwaelimisha kuhusu faida za umeme. Na kwa walio tayari wanaunganishiwa umeme na kuwashiwa papo kwa papo,” amesema Msuya.
Amesema kuwa, baadhi ya wananchi wamekuwa na changamoto za kifedha na hivyo kushindwa kumudu gharama za kutandaza nyaya ndani ya nyumba zao (wiring) ili kupokea umeme na hivyo wanawaelimisha kuhusu matumizi ya kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho ni mbadala wa wiring.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan baada ya kujua changamoto hiyo imetoa kifaa cha UMETA bure ili kuwezesha wananchi wengi kuunganishiwa umeme na gharama ambayo mwananchi anawajibika kulipia ni shilingi 27,000 tu na kifaa hiki (UMETA) ambacho ni mbadala wa wiring atapewa bure,” ameongeza Msuya.
Kwa nyakati tofauti wananchi wa vijiji vilivyotembelewa wamemshukuru na kumpongeza Mhe Rais kwa kutoa kifaa hicho (UMETA) bure kwa wananchi ambao hawana fedha kwa sasa za kutandaza nyaya ndani ya nyumba zao.
“Hii nyumba yangu ilitakiwa nifanye wiring (kusambaza nyaya ndani ya nyumba) kwa gharama ya shilingi 300,000 lakini kwa sasa nimelipia shilingi 27,000 tu. Kwa kweli nimefurahi sana maana na mimi naanza kutumia umeme huku nikiendelea kujipanga kufanya wiring. Nawashukuru sana na tunamshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Ramadhan Haruna mkazi wa Kijiji cha Chang’ombe Wilaya ya Tabora Manispaa.
Suleiman Mrisho wa Kijiji cha Mabama Wilaya ya Uyui amepongeza kampeni hiyo ya nyumba kwa nyumba ambapo anasema elimu waliyopata kuhusu matumizi ya umeme yatawasaidia kuanza kujiandaa kufanya miradi mbalimbali ya kuwaletea maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED