Utawala bora, siasa safi, elimu ziwe sekta za kimkakati - UNA

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:03 PM Jan 10 2025
Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA Tanzania) Lucas Kifyasi.
Picha Maulid Mmbaga.
Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA Tanzania) Lucas Kifyasi.

WADAU wameshauri kwamba kuelekea 2050 serikali iweke mkazi katika masuala ya utawala bora, siasa safi na elimu ziwe sekta za kimkakati katika mageuzi ya maendeleo Tanzania ili kufikiwa malengo tarajiwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yamependekezwa leo mkoani Dar es Salaam na Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNA-TANZANIA), Lucas Kifyasi, wakati wa  mkutano wa wadau wa asasi za kiraia ulioandaliwa mahususi kwaajili ya kutoa maoni ya rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkuu huyo amesema utekelezaji wa dira hiyo utafanyika miaka 25 ijayo wakati ambapo dunia itakuwa imeelekeza nguvu zake kwenye mapinduzi ya viwanda na hivyo suala la elimu litakuwa muhimu zaidi katika kuhakikisha kuwa teknolojia inakuwa thabiti na inayorithishwa kwa vizazi na vizazi.

"Pia ni muhimu serikali kuzingatia takwimu na makadirio ya kimataifa ya idadi ya watu nchini zinazosema kuwa kufikia mwaka 2050 idadi ya Watanzania itakuwa Milioni 151.3 badala ya Milioni 140 iliyopo kwenye dira pamoja na kuzingatia kushuka kwa hali ya uzazi ambayo imekuwa ikishuka kila wakati hasa katika mikoa ya Iringa na Dodoma," amesema Kifyasi.

1


Ameongeza kuwa kiwango cha uzazi nchini Tanzania kwasasa ni asilimia 4.5 huku Dodoma na Iringa ikiwa ni chini ya asilimia 3.5 suala ambalo linatishia upungufu wa idadi ya watu na hivyo kuleta athari katika maendeleo na ukuaji wa uchumi nchini.

Pia Kifyasi ameshauri ni muhimu kuimarisha na kuongeza tija kwenye sekta za elimu, ajira na uzalishaji ili kuondoa kiwango kikubwa cha utegemezi kinachofikia asilimia 87.1 kwa sasa.
2