RIPOTI MAALUMU: Matukio ya msuguano wa kijamii yanavyoangamiza misitu ya mkoa

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 09:56 AM Dec 03 2024
Matukio ya moto katika misitu yanatajwa kutishia uchumi wa Mkoa wa Njombe.
Picha:Mtandao
Matukio ya moto katika misitu yanatajwa kutishia uchumi wa Mkoa wa Njombe.

CHUKI, visasi, dhuluma, hila, wivu wa maendeleo, urinaji asali na kilimo kando ya vyanzo vya maji, maarufu vinyungu, ni chanzo cha matukio mengi ya moto katika misitu ya Njombe, uongozi wa mkoa huo umethibitisha.

Kwa mujibu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), mkoa wa Njombe ulioanzishwa rasmi mwaka 2012, unakadiriwa kuwa na hekta za misitu 664,720.83. Kati yake, misitu ya asili ina ukubwa wa hekta 263,320.83 na ya kupandwa ina ukubwa wa hekta 401,400. Misitu hiyo inachukua asilimia 31.39 ya ardhi yote ya mkoa huo.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2022/23 kulikuwa na matukio ya moto 138 katika misitu ya mkoa huo yaliyoteketeza hekta 112,299.01 za miti zenye thamani ya Sh. 400,850,754,459.16 (bilioni 400.851/-).

Mchanganuo wa TFS unaonesha kuwa kati ya matukio hayo, Halmashauri ya Wanging’ombe ilikuwa na matukio ya moto 24 yakiteketeza hekta 446.8 zenye thamani ya Sh. 5,495,466,912 Halmashauri ya Ludewa ilikuwa na matukio 35 yaliyoharibu hekta 90,832.5 zenye thamani Sh. 142,512,570, Makete ilikuwa na matukio 22 yaliyounguza hekta 3,993.51 zenye thamani Sh. 74,545,560,661.26.

Halmashauri ya Mji wa Makambako ilikuwa na matukio 10 yaliyoteketeza hekta 49.6 zenye thamani ya Sh. 925,866,708, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilikuwa na matukio 31 yaliyounguza hekta 6,381.6 zenye thamani ya Sh. 119,533,872,003 na Halmashauri ya Mji Njombe ilikuwa na matukio 16 yaliyoharibu hekta 10,573 zenye thamani Sh. 197,362,675,477.50.

Kwa mujibu wa TFS, mkoa wa Njombe mwaka 2023/2024 ulikuwa na matukio ya moto 51 yaliyoteketeza hekta 4,481.49 zenye thamani ya Sh. 5,692,025,943.50.

Mbali na kuchangia mabadiliko ya tabianchi, uchomaji moto misitu pia unatajwa kusababisha umasikini kwa wananchi wanaotegemea kilimo biashara (kilimo cha miti).

Baadhi ya wakazi wilayani Njombe waliozungumza na mwandishi wa habari hii, wanasema hakuna sheria kali ambayo inambana mwananchi moja kwa moja endapo atabainika kuchoma moto na kuunguza misitu.

"Ninadhani haipo, kama ingekuwapo sheria kali inayombana, kama vile kufungwa jela miaka kadhaa na wananchi wenzake wanakasikia 'jamani fulani aliyechoma moto ukaunguza milima na milima, amehukumiwa kifungo gerezani, ninaamini wengi wangejifunza. Lakini, hivi sasa unaona anayeunguza hana hata kitu chochote cha kulipa," anashauri Twiluma Mathias, mkazi wa wilayani Njombe.

Aneth Mwalongo, mkazi wa wilaya ya Njombe, anasema kuwa kutokana na kuwapo matukio mengi ya uchomaji misitu, baadhi ya watu wameacha kupanda miti. Wanahofia kupata hasara.

"Msitu ukishaungua, ninakula hasara. Hivyo, itafika wakati hakutakuwa tena na mbao huku kwetu kwa sababu wengi wanaunguliwa miti hiyo ya mbao ikiwa midogo ya miaka miwili, mitatu hadi mitano,” Aneth analalama.

Mkazi mwingine wa wilayani Njombe, Bushery Kilasi, anasema kuwa baadhi ya wanaochoma moto misitu, wanafanya hivyo kwa makusudi kutokana na chuki waliyonayo.

"Hivi ni vita baridi na itakuwa ya moto zaidi tuendako. Mtu anachoma makusudi na hana shida na ikitokea amekamatwa kesi inaishia ofisini kwa watendaji, mambo yanaisha huko na wewe (mkulima/mwekezaji) tayari umepata hasara," anaonya Kilasi.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kifanya, Halmashauri ya Mji wa Njombe, wilayani Njombe, Bariki Kabelege, anasema wamekubaliana kuwa na sheria ndogo zinazoelekeza kutoa fedha Sh. 20,000 kwa mtu yeyote atakayebaini kuwapo moto katika eneo lolote hata kama haujaanza kuleta madhara katika msitu husika. Kwa atakayesababisha tukio la moto, atapigwa faini ya fedha Sh. 50,000.

"Tumeamua kuwa na utaratibu huu kwa sababu kasi ya mashamba kuungua ni kubwa kwetu. Kuna matukio mengi ya moto wakati wa kuandaa mashamba, maarufu vinyungu.

"Kuanzia mwezi Julai mwaka huu mpaka sasa (mwezi uliopita), ni hekta nyingi. Lakini ni zaidi ya hekta 200 zimeteketea ambazo zilikuwa na mazao, kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo.

"Ni hasara kubwa kwa wananchi wenyewe, wawekezaji wa nje wanaokuja kuwekeza na wafanyabiashara wengine ambao kazi yao si kupanda miti au kuzalisha miti, bali kuchakata au kupata mazao ya misitu," anasema Kabelege.

Diwani wa Kifanya, wilayani Njombe, Nolasco Mtewele, anasema pamoja na kuwapo sheria ndogo zinazoelekeza hatua za kukabiliana na moto msituni, hazitekelezwi vizuri na watendaji wa serikali.

"Ninaomba vijiji vyote vinavyozunguka kata ya Kifanya vihakikishe kwenye suala la moto, vinaweka kipaumbele sana kwa sababu uchumi wetu tunaonekana tupo vizuri kutokana na misitu ambayo tunapata mbao," anasema Mtewele.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kifanya, Alberto Mkalawa, anasema wanazo sheria ndogo za kijiji zinazoelekeza, "ukihitaji kusafisha shamba kwa kuchoma moto, ni lazima wawapo watu wasiopungua 10 wakati wa uchomaji moto".

Hata hivyo, Mwenyekiti Mkalawa ana angalizo lenye ushuhuda, akisema, "Tukaja kugundua changamoto kwamba mwenye kibali cha kuandaa shamba, akishapata watu 10 wa kumsaidia kudhibiti moto, anabeba pombe anakwenda nayo huko shambani.

"Madhara yake ni kwamba watakunywa ile pombe, hawatakuwa makini kuzingatia ule moto namna walivyochoma lile shamba, na isivyo bahati inatokea wanashindwa kudhibiti moto, hivyo kuangamiza msitu jirani na shamba husika."

Mhifadhi wa Misitu Mwandamizi wa TFS Wilaya ya Njombe, Audatus Kashamakula, anasema uchomaji misitu Njombe unasababishwa na mambo mengi yanayojumuisha visasi na chuki, urinaji asali na uandaaji mashamba.

Kashamakula anataja vyanzo vingine vya matukio ya moto misituni Njombe ni uchomaji mkaa na uchomaji mashamba ya miti kwa makusudi ili kuwakomesha wamiliki wa mashamba hayo ikiwa kuna migogoro ya kifamilia. Hasara huwakumba hata wasiohusika na mgogoro husika kwa kuwa moto huunguza hadi mashamba yaliyo jirani.

"Wananchi wengi wa Njombe wana utamaduni wa kizamani wa kuandaa mashamba kwa kuchoma moto pasi na mikakati mizuri ya kuudhibiti," anasema Kashamakula.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, anaelekeza hatua za haraka zichukuliwe ili kukabiliana na majanga ya moto yanayosababisha hasara kubwa kwa jamii na taifa.

Maelekezo yake kwa watendaji walio chini yake ni kwamba kila wilaya iweke mikakati ya kuvifikia vijiji vyote kwa ajili ya kutoa elimu ya kukabiliana na matukio ya moto yanayoteketeza misitu.

"Lazima tufanye kazi kwa pamoja ili tuje na majawabu kwenye suala la moto katika mashamba yetu ya misitu, ni hasara ya mabilioni. Hatuwezi tukaliacha hili jambo, mapato ya mkoa wa Njombe kwa sehemu kubwa yanategemea ushuru kwenye mazao ya misitu; shamba au mbao, magogo, mabanzi, mirunda, mkaa na guzo. Hivyo ni lazima tujue kwamba uchumi wetu upo hapa.

"Mtu anapokwenda kuandaa nusu ekari ya shamba la mahindi, akichoma kwa ajili ya kusafisha shamba, kuna mtu mwingine huku anapoteza ekari 500 za miti.

"Hivyo, ni lazima huyu mtu ajue hii hasara atakayokuwa ameisababisha, kuna watu wanapata kiharusi, kuna watu huko wanachanganyikiwa kwa sababu ya tatizo hili," anaonya Mtaka.

Ofisa Ukaguzi wa Usalama wa Moto Mkoa wa Njombe kutoka Jeshi la Zimamoto, Hilary Kobero, anasema wanaendelea kutoa elimu ya uandaaji mashamba pasi na kusababisha hasara.

"Miongoni mwa njia ambazo wanapaswa kuzifuata kwelikweli ni zile sheria ndogo ambazo zimewekwa katika mamlaka za serikali za vijiji. Sheria ziko wazi, zinasema muda, hali ya hewa ambayo inapaswa ifuatwe lakini pia na idadi ya watu wanaopaswa wawapo wakati wa kuwasha moto," anasema Mkaguzi Kobero.

Anasisitiza kuwa wananchi wakiona upepo ni mkali, hawapaswi kuchoma moto mashamba yao siku hiyo hata kama wamepewa kibali.

Mkaguzi Kobero pia anatoa rai kuchongwa barabara za kutosha kutoka shamba moja hadi lingine, ziwe na upana na mita sita, hasa kwa mashamba ya miti ili kusaidia kuzuia moto kutoka shamba moja kwenda lingine.

Vilevile, mkaguzi huyo aliwataka maofisa kilimo mkoani Njombe kutoa elimu kwa wakulima ili watumie njia mbadala kuandaa mashamba. Waache kuandaa mashamba yao kwa kuchoma moto.