RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kuunga mkono shughuli mbalimbali za Serikali yake, ikiwemo Shamrashamra za Miaka 61 za Mapinduzi ya Zanzibar, ilikodhamini na kushiriki Siku ya Kitaifa ya Mazoezi na Michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Pongezi hizo amezitoa mapema Jumatano Januari Mosi, wakati Dk. Mwinyi alipoongoza maelfu ya Wazanzibar kushiriki Siku ya Kitaifa ya Mazoezi Zanzibar kwenye Uwanja wa mnazi mmoja wilayani Wete mkoa wa kaskazini Pemba, ambayo ni sehemu tu ya shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi ya Matukufu Zanzibar, ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12.
Dk. Mwinyi ameipongeza NMB kwa kufadhili mazoezi hayo, ambako ilikabidhi ‘tracksuit’ 100 za kuvaa viongozi, zikiwa na thamani ya Sh. Mil. 9, huku ikidhamini Michuano ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup 2025) kwa Sh. Mil. 50, mchango uliomsukuma Rais Mwinyi kuiomba taasisi hiyo kudumisha mashirikiano hayo.
“Niwashukuru sana Benki ya NMB kwa kuendelea kuunga mkono shughuli mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na hata Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wameshiriki pakubwa katika tukio hili muhimu kwa mustakabali wa Afya za Wazanzibar, wameshiriki na kutufanya tupendeze kwa sare walizotoa.
“Hongereni sana NMB na kimsingi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatambua, inathamini na kujali mchango wenu mkubwa kwa maendeleo na ustawi wa Wazanzibar. SMZ inaamini mtaendelea kushirikiana nayo katika kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa,” alisema Dk. Mwinyi katika mazoezi hayo.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Naima Said Shaame, alisema benki yake imekuwa mshirika mkubwa wa shughuli mbalimbali za Serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, inakodhamini kwa miaka 12 sasa.
“Huu ni mwaka wa 12 sasa NMB inashirikiana na SMZ kufanikisha Sherehe za Mapinduzi, ambako mwaka huu tumekabidhi ‘tracksuit’ za mazoezi 100 zenye thamani ya Sh. Mil. 9, tukiamini kwamba mchango huo utakuwa chachu ya kuhamasisha mazoezi vizsiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.
“Pia, tumetoa Sh. Mil. 50 kudhamini Kombe la Mapinduzi, udhamini ambao pamoja na ‘tracksuit’ hizo, tunaamini kwamba, ni kilelezo na uthibitisho wa dhati kuwa NMB inathamini michezo, kwani afya zetu zinaimarika zaidi kupitia michezo na uimara wa afya ndio chachu ya kukua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Ni fahari kubwa kwetu kuendelea kushirikiana na Serikali kwa miaka 12 ya NMB kuwa sehemu ya ukamilifu wa matukio hayo kwa kipindi chote hicho," alisisitiza Naima katika hotuba yake mbele ya maelfu ya Watanzania walioshiriki wakiongozwa na wenyeji wa Kisiwa cha Pemba.
Mapema juzi, NMB kupitia Meneja wa NMB tawi la Zanzibar, Ahmed Jumaa Nassor, alimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajabu, ‘tracksuit’ hizo 100 na hundi ya mfano yenye thamani ya Sh. Mil. 50 za Udhamini wa Kombe la Mapinduzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED