Wauza vyakula jirani na mitaro, mzingatie afya za mnaowahudumia

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 07:54 AM Sep 19 2024
 Wauza vyakula
Picha: Mtandao
Wauza vyakula

MARA zote kanuni za afya zinajulikana, kwamba unajijali mwenyewe na wenzako, wawe wanafamilia au walio jirani na mahali uliko katika tafsiri pana, kama vile mahali unakofanya kazi zako.

Usafi unatafsiri uhai wa mwanadamu. Hilo lililtumiwa sana na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, katika siku za kwanza za uhuru wa nchi, azma kuu ikiwa kuiunda jamii yenye uhakika na uhai wake. 

Mwendelezo wake haujawahi kutelekezwa kitaifa hadi jamii ilikofika, hatua mbalimbali za bidii zinaendelezwa kwenye dhana ya ubora wa afya kitaifa, binadamu wakigawanywa katika makundi mbalimbali kama vile watoto, wazee na kimamama kila kundi na vipaumbele vinavyogusa nafsi zao. 

Hali kadhalika, kuna aina ya mazingira yanayojitokeza kitaifa na dunia katika hilo, juhudi za kitaifa zikisaidiwa sana na miongozo ya kimataifa, hasa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Imekuwa kawaida kila mara tunasikia mlipuko wa magonjwa ama mapya au yaliyokuwa yamejificha na yanaibuka tena. Ndiyo maana hivi karibuni tumekuwa kwenye pilika za kukwepana na maradhi ya corona mitaani kwetu, vivyo hivyo kwingineko duniani. 

Tukirejea mazingira ya mahali tuliko na tunaishi, tunashuhudia mvua kunyesha mfano mjini Dar es Salaam, baadhi ya maeneo yenye mitaro imekuwa ikijaa maji, huku wengine wakitumia mvua hizo kuzibua ‘chemba’ zao za vyoo zilizojaa. 

Hata hivyo, katika uhalisi wa maisha, ujio wa mvua ni baraka za asili kutoka kwa Mungu, mvua zisiponyesha, jamii huungana na viongozi wa dini katika maombi ili mvua iweze kunyesha. 

Pamoja na hayo, mvua inaponyesha, kuna watu wanaofurahia kupata maji, kwamba ni mbadala wa kununua maji. Pia, wapo wanaopumzika na jukumu la kumwagilia maji bustanini. 

Lakini kuna wenzao wanaoangukia vilio, kwamba miundombinu yao inaharibika. Wenye visa hivyo vinawaangukia hata wale Wamachinga, ambao wanaweka bidhaa zao chini na mvua inaponyesha hubomoa utaratibu wote. 

Sasa turudi kwa wenzetu wafanyabiashara maeneo ya pembezoni ya mitaro, ambako mvua zikinyesha mitaro kujaa maji, maji hayo hutoa harufu mbaya na kuchangia kuzibuliwa mitaro penye mazingira yao. 

Ukiangalia mitaro iliopo pembezoni barabarani kuna wafanyabiashara katika hiyo mitaro iliyozibika, kutokana na uchafu kukusanyika. 

Mitaro inapoziba, ambayo ni hali ya kawaida katika sehemu nyingi unakuta mitaro imeziba na wafanyabiashara hawaoni jirani, baadhi kana kwamba hawaoni au wanataabika nalo, wanaendelea na biashara, huku uchafu na harufu yake nayo inaendelea. 

Pale mitaro inapozibuliwa, unakuta harufu mbaya inatawala maeneo jirani na kuna mazingira hunishangaza kuona hakuna hisia  za wafanyabiashara kukereka, tena wauzaji vyakula na matunda. 

Sasa kwa kufanya hivyo kunachangia kuharibu afya ya watu, hasa wateja wa vyakula hivyo. 

Napenda niwaeleze ndugu zangu wauza matunda na vyakula, muwe na subira. Kama mitaro imejaa na hali ya afya hapo si salama, jambo jema hasa ni kutafuta maeneo mbadala ya kuendeleza biashara walau kwa muda na sio kuendelea kudumu hapo pasipofaa. 

Ila kwa wenye mamlaka, hususan ngazi ya halmashauri, elimu ya kina iendelee kutolewa kwa wahusika kuhusu mustakabali wa afya, maana ndio wadau wenu wa karibu. 

Elimu hiyo itasaidia kuwaandaa wafanyabiashara, penye changamoto namna mbalimbali, waliko katika maeneo hayo kibiashara, wajue nini cha kufanya ili kuweza biashara iendelee, sambamba na mazingira mazuri.

 Aina hiyo ya ushuhuda si wa watu wazima pekee, pia wanafunzi nao unakuta wamefurika katika vibanda vya wafanyabiashara kunakouzwa milo na vitafunwa, katika mazingira yasiyofaa. Hapo kundi hilo nalo llinahitaji elimu stahiki kutolewa kulinda afya za walaji.