Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Alhaji Batenga, amesema serikali inaendelea kutekeleza mikakati kabambe ya kuimarisha shughuli za uchimbaji madini wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa kituo cha umeme (substation) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 90, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa wachimbaji na shughuli nyingine za maendeleo.
Akizungumza na timu ya Madini Diary tarehe 9 Oktoba 2025, Batenga alisema kituo hicho kitajengwa katika eneo la Makongorosi – Chunya, na kitahudumia maeneo ya Chunya na Mkoa wa Songwe. Alitaja miradi itakayofaidika na mradi huo kuwa ni mgodi mpya wa Shanta-New Luika, mtambo wa uchenjuaji wa Anglo De Beers uliopo mpakani mwa Chunya na Songwe, pamoja na mgodi wa Porcupine North uliopo katika eneo jipya lililopanuliwa.
Kwa sasa, alisema, wilaya hiyo inatumia megawati 9 pekee huku mahitaji halisi yakiwa si chini ya megawati 90. “Kupitia kituo hiki tutaanza kuzalisha megawati 45 awamu ya kwanza. Lengo ni kuwezesha uchimbaji wa kisasa kwa gharama nafuu na kuchochea uwekezaji zaidi.
Wachimbaji wetu wanahitaji sana umeme, na nimepokea maombi mengi ya kufikishiwa huduma hii — jambo ambalo nitalisimamia kwa nguvu zote,” alisisitiza Batenga.
Batenga aliutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa kipaumbele cha kusambaza umeme katika maeneo yenye shughuli za madini, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija.
Alisema upatikanaji wa nishati ya uhakika utavutia wawekezaji zaidi, hasa ikizingatiwa kwamba Chunya imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za madini. Aidha, alitaja ujio wa kampuni ya Anglo De Beers, ambayo ina baadhi ya leseni zake Chunya na tayari imeanza uchimbaji katika eneo la Mbangala – Songwe.
Akitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Batenga alimsifu kwa kuliweka sekta ya madini katika vipaumbele vya serikali, hususan kwa wachimbaji wadogo. Alibainisha kuwa zaidi ya leseni 1,500 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo wilayani humo, na akaomba leseni zisizoendelezwa zirudishwe ili ziweze kutolewa kwa wenye nia ya kuziendeleza.
Katika hatua nyingine, Batenga aliomba Wizara ya Madini kuongeza tafiti za kisayansi ili kubaini maeneo mapya yenye madini, akipongeza hatua ya wizara kutoa mitambo ya uchorongaji miamba kwa wachimbaji. Hata hivyo, alishauri kupatikana kwa mitambo yenye gharama nafuu zaidi ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kumudu utafiti.
“Sisi hatuchimbi dhahabu pekee,” alisema.
“Kwa sasa tuna kiwanda cha kuchenjua shaba, hivyo nawahimiza wachimbaji waanze pia kuangalia fursa katika madini hayo.”
Akizungumzia uchumi wa wilaya, Batenga alisema Chunya imegawanyika katika tarafa mbili zenye utajiri tofauti: Kiwanja, inayojulikana kwa shughuli za madini, na Kipambawe, inayojihusisha zaidi na kilimo cha tumbaku.
“Madini hayapo kabisa Kipambawe, na vivyo hivyo tumbaku haistawi Kiwanja. Kila tarafa ina utajiri wake wa kipekee,” alieleza.
Kwa mujibu wa Batenga, sekta za madini na kilimo cha tumbaku kwa sasa zinachangia asilimia 60 ya fedha za maendeleo katika mfuko mkuu wa Serikali, ikilinganishwa na asilimia 40 miaka ya nyuma.
“Tunatarajia ndani ya miaka mitano ijayo Chunya itachangia hadi asilimia 80, kutokana na ongezeko la mapato ya madini na tumbaku. Kwa sasa Halmashauri inapata takribani shilingi bilioni 5 kila mwaka kutokana na sekta hizo mbili kuu,” alihitimisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED