Wananchi watoa machozi mbele ya mgombea Urais Zanzibar

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:20 PM Sep 21 2025
Wananchi watoa machozi mbele  ya mgombea Urais Zanzibar
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Wananchi watoa machozi mbele ya mgombea Urais Zanzibar

WANANCHI wa Kijiji cha Mbuyu Tende, Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja wamemwaga machozi mbele ya Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kwa kile walichoeleza wameporwa ardhi yao ya urithi.

Aidha, wamedai kuwa ardhi hiyo kwasasa inamilikiwa na wageni ambao ni wawekezaji, huku wao wakikosa eneo la kufanya shughuli za uzalishaji. Wakizungumza mbele ya Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman wazee hao walieleza kuwa wameishi katika mateso ya kuona ardhi yao ikitolewa kwa wageni, huku wao wakibaki bila manufaa yoyote. 

“Ardhi tuliyoirithi kutoka kwa mababu zetu sasa imegeuzwa mali ya wageni. Hata ajira zinazotokana na hoteli hizo zimepewa wageni wao, sisi tumebaki bila kitu,” walisema kwa uchungu. Waliongeza kuwa hata bahari ambayo ilikuwa tumaini la maisha yao, sasa imegeuzwa eneo la marufuku. 
Walisema kuna sehemu za bahari ambazo haziwezi kufikika tena kwa wavuvi wa kienyeji, kwa sababu zinalindwa na askari maalumu wenye silaha. “Tumegeuzwa kuwa wageni katika nchi yetu wenyewe, tumebaki bila ardhi, bila ajira, na sasa hata bahari imeporwa,” alisema kijana mmoja kwa hasira huku akishangiliwa na wananchi wenzake.

Akijibu malalamiko hayo, Mgombea Urais Othman Masoud aliwaahidi wananchi wa Mbuyu Tende kuwa ukombozi wao umekaribia.Alisisitiza kuwa katika utawala wake, ardhi ya Mzanzibari haitachukuliwa tena kwa kisingizio cha uwekezaji usio na faida kwa wananchi. “Hakuna tena dhulma ya ardhi. Hakuna tena mzanzibari kunyimwa nafasi ya ajira.  Hii nchi ni yetu na lazima iwe kwa ajili ya wananchi wake kwanza,” alisema Othman.

Aidha, ameahidi kuwa serikali itakayoongozwa naye itasimamia uwekezaji rafiki kwa wananchi, utakaolinda utu na heshima ya Mzanzibari, na kuhakikisha wazawa wanapewa kipao mbele katika kila sekta ya uchumi. “Tutajenga Zanzibar mpya yenye haki, yenye usawa na yenye kuthamini wananchi wake kuliko wageni,” amesema.Aidha, wananchi walimpongeza kwa kauli hizo, wakieleza kuwa kauli ya Othman Masoud imeamsha matumaini mapya ya ukombozi wa ardhi na heshima ya Mzanzibari.