Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuwa Serikali atakayoiongoza itaweka historia mpya ya kuthamini walimu wa madrasa kwa kuwajumuisha rasmi katika mfumo wa malipo ya Serikali, hatua itakayowaondoa kwenye maisha magumu wanayopitia kwa sasa.
Akizungumza na walimu wa madrasa katika mkutano uliofanyika Wilaya ya Chake Chake, Pemba, Othman alisema walimu hao wamekuwa nguzo muhimu katika kujenga maadili, misingi ya dini, na malezi bora kwa watoto wa Zanzibar, lakini Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuwaenzi_ ipasavyo.
Alisema kiuhalisia walimu wa madrasa walipaswa kuwa kundi la tatu linalopewa kipaumbele na Serikali kutokana na nafasi yao ya kipekee katika jamii.
Aliongeza kuwa ndani ya Serikali yake, walimu wote wa madrasa waliosajiliwa watapata mshahara kama walimu wengine wa Serikali.
Amesema Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha inaunda mfumo maalumu wa maslahi ya walimu wa madrasa, ikiwa ni pamoja na michango ya hifadhi ya jamii na bima ya afya, ili kuimarisha ustawi wao na kuongeza ari ya kufundisha.
Othman aliongeza kuwa walimu hao ndio wanaowaandaa watoto katika msingi wa maisha, kabla hata hawajaingia katika elimu ya msingi, hivyo ni lazima Serikali iwaone kama msingi wa maadili ya taifa.
Amesema walimu hawa wanawafundisha watoto hofu ya Mungu, uadilifu na upendo. Hawa ndio wanaojenga jamii yenye maadili. Serikali isiyowajali ni Serikali isiyojali mustakabali wa taifa.
Kwa upande wao, baadhi ya walimu wa madrasa walimshukuru mgombea huyo kwa kuonyesha moyo wa kuthamini kazi yao.
Suleiman Abdalla Khatib, Mwalimu wa Madrasa ya Madungu, alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa kipato cha uhakika.
Alisema wakati mwingine wanajikuta wakilazimika kuchangisha kila mwanafunzi shilingi elfu tatu ili angalau wapate fedha za matumizi ya mwezi.
Hata hivyo, bado kuna wazazi wanaoshindwa kuchangia kwa sababu ya umasikini.
Naye Harith Suleiman Khalifa aliongeza kuwa wazazi wengi siku hizi wamekuwa wakihamasisha watoto wao kujikita zaidi kwenye elimu ya dunia pekee, huku wakisahau umuhimu wa elimu ya dini.
Alisema mzazi anafurahia kuona mtoto wake anakwenda skuli hadi jioni, lakini akihimizwa kwenda madrasa muda wa ziada, anaona ni mzigo.
Alisema huo ndio mfumo unaowaharibu vijana wengi kukosa maadili na kupelekea tabia za ufisadi wanapopewa dhamana.
Katika hotuba yake ya kuhitimisha, Othman alisisitiza kuwa Serikali ya ACT Wazalendo italenga kujenga Zanzibar yenye heshima, utu na usawa, ambapo kila kada ya elimu, ikiwemo madrasa, itapewa nafasi ya kuheshimika na kuthaminiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED